Simba Inakutana Na Nguli Wa Afrika

MWAKA 2003, Simba ikiwa na kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji vijana na wazoefu ilifanikiwa kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini safari yao haikuwa nyepesi.

Katika hatua ya awali Simba iliitoa Botswana Defence Force XI ya Botswana, Raundi ya Kwanza ikaitoa Santos ya Afrika Kusini. Baada ya hapo ikakutana na Zamalek ya Misri ambao ndiyo walikuwa mabingwa watetezi.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawassa anasimulia kwa ufupi juu ya mchezaji aliyekuwa staa wa Zamalek, Hossam Hassan.

Pawassa anasema: “Kipindi hicho ndiyo Zamalek ilikuwa imetoka kupewa ubingwa, tukapangwa kukutana nao katika Raundi ya Pili ambayo ni ya mtoano kabla ya kuingia Hatua ya Makundi.

“Kwanza kabla ya kuelekea mchezo huo tulipewa presha kubwa sana kwa kuwa Zamalek walikuwa katika ubora wa juu, nakumbuka kabla ya mchezo huo nilipata takribani SMS zaidi ya 250, lakini nyingi kati ya hizo zilikuwa ni kuhusu Hossam Hassan.

“Niliambiwa naenda kukutana na mchezaji bora wa michuano ya Afrika pia alikuwa mfungaji bora wa michuano ya Mataifa ya Afrika.
“Sikuwahi kuwa na majukumu mazito kama niliyopewa kuelekea mchezo huo. Nashukuru Mungu katika mchezo wa kwanza nilifanikiwa kumdhibiti (Hossam), ilipofika dakika ya 75 akanipiga kiwiko na kunichana juu ya jicho, nilishonwa nyuzi sita na kufanikiwa kuendelea na mchezo… Jamaa alikuwa hatari.”

Hiyo ni sehemu ya simulizi ya Pawassa, baada ya hapo Simba walifanikiwa kusonga hatua ya makundi kwa penalti kutokana na matokeo ya bao 1-1 katika michezo yote miwili.
Hossam Hassan ni nani?
Ni straika wa zamani ambaye ana heshima kubwa kwenye soka la Misri na Afrika kwa jumla. Anatarajiwa kukutana na Simba, wiki ijayo akiwa katika sura na majukumu tofauti kwa mara nyingine.
Hossam ambaye ana umri wa miaka 51 ni kocha mkuu wa Al Masry ya Misri ambayo itakipiga dhidi ya Simba katika Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hizo zitakutana Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jini Dar kisha zitarudiana wiki moja na nusu baadaye nchini Misri.
Hossam ambaye enzi zake alijulikana kwa uwezo wake wa kufunga mabao, kucheza soka la nguvu na kuwa mhamasishaji anapokuwa uwanjani na hata akiwa nje ya uwanja, ndiye mtu maarufu zaidi katika msafara huo wa Al Masry utakaotua nchini.

Comments

Popular posts from this blog