Hii ndio Mikoa vinara wa vifo vinavyosababishwa na wivu wa mapenzi
Mikoa ya Singida na Tabora imebainika kuwa vinara wa matukio ya mauaji baina ya wanandoa katika miaka ya 2016 na 2017, kwa kuwa na matukio 314 kutokana na wivu wa mapenzi na ugomvi wa kifamilia.
Takwimu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kupitia Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa kwa gazeti la Habari Leo, zinaonesha kuwa, mwaka 2016 kulikuwa na mauaji 151 baina ya wanandoa.
Mwaka 2017 mauaji hayo yaliongezeka na kufikia 163 ambayo ni nyongeza ya mauaji 12 sawa na asilimia 7.9.
Zinasema Mkoa wa Singida ulikuwa na matukio 27 ukifuatiwa na Tabora uliokuwa na mauaji 26 baina ya wanandoa.
Mikoa mingine iliyofuata kwa wingi wa matukio ya wanandoa kuua wenza wao na idadi kwenye mabano ni Geita (25), Mwanza (21), Kagera (20) Mbeya 19 na Shinyanga (18).
Mwaka 2016 Mkoa wa Shinyanga uliongoza kwa wanawake saba kuua waume zao, ukifuatiwa na Tabora sita huku mikoa ya Singida na Iringa ikiwa na matukio manne ya mauaji. Kwa mwaka 2017, mikoa ya Mwanza na Kagera iliongoza kwa wanawake kuua waume zao kwa matukio manne kila mmoja.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa mwaka 2016 Mkoa wa Geita uliongoza kwa matukio 17 ya wanaume kuwaua wake zao, ukifuatiwa na Singida na Dodoma kwa matukio manane kila mmoja, huku mikoa ya Tabora na Mbeya ikiwa na matukio saba kila mmoja.
Katika mwaka 2017, Mkoa wa Singida uliongoza kwa wanaume kuua wake zao 15 ukifuatiwa na mikoa ya Mwanza, Songwe na Mbeya iliyokuwa na matukio kumi kila mmoja. Tabora ulikuwa na matukio tisa huku mikoa ya Shinyanga na Kagera ikiwa na matukio manane kila mmoja.
Comments
Post a Comment