DIAMOND KULAMBA SHAVU KOMBE LA DUNIA SIRI YAFICHUKA!

DAR ES SALAAM: Nyuma ya tukio la Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kulamba shavu la kuimba wimbo wa uzinduzi wa Michuano ya Kombe la Dunia 2018, Ijumaa Wikienda limebaini siri iliyochangia uteuzi wake huo.
Katika uchunguzi mdogo uliofanywa na gazeti hili, mambo matatu makubwa ambayo ndiyo sababu kubwa iliyowafanya waandaaji wampe kipaumbele rais huyo wa Wasafi Classic Baby (WCB).
Ijumaa Wikienda lilibaini kuwa, jambo la kwanza lililochangia Diamond ateuliwe ni bidii ya uongozi wake chini ya Sallam SK. Sallam ametajwa kuwa miongoni mwa mameneja ambao wana ‘connection’ nyingi za vituo vikubwa vya redio na televisheni ambavyo hucheza nyimbo za Diamond duniani.
Ilielezwa kuwa, connection hizo ndizo zilizochangia kuwashawishi waandaaji wa michuano hiyo wakati walipokuwa wanaangalia ni wasanii gani wa Afrika ambao wana uwezo na ushawishi mkubwa, wakampendekeza Diamond.
Mbali na hilo, jambo lingine lililochangia Diamond ateuliwe na kushiriki katika uzinduzi wa mashindano hayo makubwa kuliko yote duniani ni kitendo cha yeye kuwa miongoni mwa wasanii ambao wanatikisa kwa Afrika Mashariki, Magharibi na Kati kwa sasa.
Ilibainika kuwa, Diamond amelikamata vizuri soko la Afrika Mashariki, akaenda mbele zaidi na kufanikiwa kuwapoteza wakali wanaotamba Afrika wakiwemo P Square, Davido, Tekno, Wizkid, Tiwa na Yemi Alade.
Jambo la tatu ambalo pia ndilo lilichangia kwa kiasi kikubwa Diamond kupata shavu hilo ni kolabo zake kubwa na wasanii wakubwa wa Marekani, ikiwemo wimbo Wakawaka aliofanya na Rick Ross na Marry You aliofanya na Neyo.
Ilielezwa kuwa, kolabo hizo zimekuwa chachu kwa waandaji wa michuano hiyo kutopata ugumu wa kufahamu kazi za Diamond kwani waliweza kumuona kupitia ngoma hizo na kujiridhisha kwamba ana kipaji.
Pamoja na mambo hayo matatu, Ijumaa Wikienda pia lilibaini sababu nyingine ya ziada iliyowashawishi waandaaji kumteua Diamond ni rekodi ya shoo zake zilizopo kwenye Mtandao wa YouTube.
Diamond amekuwa miongoni mwa wasanii ambao wamekuwa wakijaza watu wengi katika shoo mbalimbali ndani na nje nchi. Shoo hizo zimetajwa pia kuwa kivutio kwa waandaaji.
Akizungumza na mwanahabari wetu kuhusiana na uteuzi huo, Diamond alisema kuwa, hata yeye hajui hasa ni nini kilisababisha, lakini uteuzi ulikuja kwake kama ‘surprise’.
“Ukiniliza hata sijui ni nini hasa waliangalia hadi kuniona mimi, lakini ghafla tu nilishangaa kuona simu, naambiwa nimeteuliwa,” alisema Diamond.
Mkali huyo kutoka Tandale jijini Dar, anatarajia kurekodi wimbo maalum wa uzinduzi wa Kombe la Dunia uitwao Colour akishirikiana na wakali wengine kama Jason Derulo na Cassper Nyovest.
Wimbo huo unatarajiwa kuachiwa Machi 16, mwaka huu wakati michuano hiyo ya Kombe la Dunia ikitarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni, mwaka huu nchini Urusi.
Kwenye mashindano hayo, Diamond anatarajia kukutana uso kwa uso na mastaa wakubwa wa soka duniani akiwemo Paul Pogba (Ufaransa), Cristiano Ronaldo (Ureno), Lionel Messi (Hispania) na wengine kibao.
STORI: Mwandishi Wetu, IJUMAA WIKIENDA

Comments

Popular posts from this blog