Uwoya, Aunt Ezekiel Wamchokonoa Shonza
DAR ES SALAAM: KITENDO cha wasanii wa filamu, Aunt Ezekiel Grayson Gwantwa ‘mama Cookie’ na Irene Pancras Uwoya kutupia picha mtandaoni zikionesha wakiwa wanaogelea huku maeneo nyeti ya miili yao yakiwa wazi, kimetafsiriwa na wadau mbalimbali ni kama ‘kuishika sharubu’ serikali.
Mwanzoni mwa wiki hii, picha za wasanii hao wakiwa ndani ya majakuzi sehemu tofauti na kwa nyakati tofauti zimeleta hisia tofauti kwa jamii huku wengine wakienda mbele kwa kusema kitendo hicho ni kukaidi agizo la Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kupitia naibu waziri wake, Juliana Daniel Shonza aliyepiga marufuku picha za utupu mitandaoni.
Baada ya kuvuja kwa picha hizo, waandishi wetu waliwatafuta wasanii hao kupitia simu zao za mkononi ili kusikia utetezi wao juu ya jambo hilo.
“Picha hiyo niko lokesheni (eneo la kuigizia), sasa sioni kama kuna tatizo kuonesha mtandaoni picha ya namna hiyo,” alisema Irene Uwoya.
Kwa upande wa Aunt Ezekiel, mazungumzo yake na mmoja wa waandishi wa habari hii yalikuwa hivi;
Mwandishi: Kuna picha umeweka mtandaoni unaoga kwenye jakuzi, sasa huoni kama unapingana na zuio la serikali?
Aunt Ezekiel: Sasa umenipigia simu ili uandike gazetini?
Mwandishi: Ndiyo, naomba ufafanuzi wako tafadhali maana taaluma ya habari inanitaka kukupa haki ya kukusikiliza (balancing).
Aunt Ezekiel: Sasa mbona unapiga kwenye WhatsApp kwa sababu ni bure au huna pesa ya kupiga kawaida? (MB nazo ni gharama pia), kisha anakata simu.
MAONI YA WADAU
Baada ya kumalizana na wasanii husika, waandishi wetu walizungumza na baadhi ya wadau wa sanaa na burudani ambao walitoa maoni yao juu ya kitendo hicho.
“Unajua sanaa yetu inakufa kwa sababu nyingi sana, wasanii wetu hawajielewi, kitendo cha kuoga kinamaanisha usiri na ndiyo maana kuna mabafu, unawezaje mtu kujipiga picha huku unaoga kisha kutupia picha hizo mtandaoni? Bado tunajiuliza ni kwa nini filamu zetu zimekosa msisimko! Sababu ni kama hizo,” alisema mama Jovin, mkazi wa Sinza –Kwaremi jijini Dar.
Naye Boaz Katemi wa Makumbusho alisema: “Naona siyo sawa, huko mtandaoni wanapita watu wengi wakiwemo watoto na wenye heshima zao kwenye jamii, sasa msanii ambaye ni kioo cha jamii, kuweka picha za namna hiyo mtandaoni inabidi wabadilike kwa kweli.”
WAZIRI SHONZA ANASEMAJE?
Gazeti hili lilimtafuta waziri Shonza kupitia simu yake ya mkononi ambapo alikata na kumtaka mwandishi wetu amtumie ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) lakini alipotumiwa na kuelezwa suala zima, hakujibu chochote hadi tunakwenda mtamboni.
Stori: Brighton Masalu na Imelda Mtema, Amani
Comments
Post a Comment