UTAPELI MPYA FEDHA KWENYE SIMU YAKO WATIKISA NCHINI!

IGP Sirro.

BADO wizi wa fedha za kwenye mitandao ya simu unaendelea kutikisa nchini ambapo kwa sasa njia mpya imeibuka ambayo unaibiwa fedha kwenye simu yako ukiwa nayo mkononi.
Wakizungumza na Risasi Mchanganyiko baadhi ya wananchi walilalamikia utapeli huo na kusema wameibiwa fedha zao ambazo zilikuwa kwenye simu zao.

Mmoja wa wananchi hao, Agatha John wa Mwenge jijini Dar alisema aliibiwa fedha zake shilingi 60,000 baada ya kupigiwa simu na mtu ambaye hamfahamu aliyemtaja jina lake kiufasaha na kumdanganya kwamba yeye ni ofisa wa mtandao wa simu anaoweka fedha zake.
“Mtu huyo aliniambia kuna zawadi kemkem zitatolewa na mtandao huo kwa wateja ambao wana fedha zaidi ya shilingi 50,000 hivyo alinishauri nimtajie namba yangu ya siri ili fedha na zawadi ziweze kutumwa ndani ya siku tatu,” alisema Agatha.

Aliongeza kwamba baada ya kumtajia namba zake za siri aliamini kwamba fedha zake zitakuwa salama kwa sababu simu na kadi yake anayo yeye, hivyo alidhani kuwa si rahisi kuibiwa.
“Baada ya siku tatu niliangalia salio na kukuta fedha zangu zote shilingi 60,000 zimekombwa. Nilihuzunika sana na sikuwa na pa kwenda kushitaki lakini nikawa najiuliza yule mtu alijuaje jina langu kama siyo mtu wa kampuni hiyo ya simu?” alihoji Agatha.
Naibu Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Kimtandao wa Polisi, ACP Joshua Mwangasa alipoulizwa juu ya wizi huo alisema unatokana na wananchi wengi kukosa elimu ya mitandao.

Eng. James Kilaba.

Kamanda Mwangasa amewataka wananchi kuwa makini na kuachana na watu wasiowafahamu kuwapa taarifa zozote za simu zao na amewaomba viongozi wa makundi ya mtandao wa WhatsApp kutoa taarifa pindi uhalifu unapofanyika katika makundi yao kwani kwa kiasi kikubwa makundi hayo yamekuwa yakitumika kusambaza taarifa za uongo.
Aliwataka watu ambao wametapeliwa kwenye mitandao ya simu kufika polisi ili kutoa taarifa waweze kusaidiwa badala ya kuhofia.

Naye Ofisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Philip Filikunjombe alisema utapeli huo upo na kuwataka wananchi kutotoa taarifa za simu zao kwa mtu yeyote.
Alisema wananchi wanahitaji kupewa elimu za mitandao lakini hilo linashindikana kutokana na kukosekana kwa wataalamu kwani waliopo ni wachache.

“Kuna kazi ngumu sana ya kuelimisha wananchi na kuwafanyia semina ni kitu ghali sana hivyo wananchi popote walipo wasikubali kutoa taarifa za simu zao kwa mtu yeyote hata ajitambulishe vipi,” alisema Filikunjombe.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya watumiaji wa huduma na bidhaa Kutoka TCRA, Thadayo Ringo, mamlaka hiyo inatarajia kufanya majaribio ya kusajili laini za simu kwa kutumia vidole kutokana na kuzuka kwa changamoto mbalimbali kwa watoa huduma kutokana na utolewaji wa taarifa zisizo sahihi katika usajili, jambo ambalo litasaidia kuzuia wizi mitandaoni.
STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko.

Comments

Popular posts from this blog