Mtanzania Akamatwa na Dhahabu ya Bilioni 2, Nairobi

MWANAMME mmoja anayedaiwa kuwa ni raia wa Tanzania amekamatwa na maofisa wa forodha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi nchini Kenya, akisafirisha dhahabu ya thamani ya dola milioni moja (sawa na zaidi Tsh. Bilioni 2) taarifa zinasema.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 46 anadaiwa kuingia Nairobi akitokea mkoani Mwanza, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) na alikuwa safarini kuelekea Dubai.

Gazeti la Nation limesema mtuhumiwa huyo ambaye jina lake halijajulikana hadi  sasa, aliwasili uwanja wa JKIA, Ijumaa, Februari 16 na  ndege ya Precisio Airlines akitaka kuunganisha na ndege ya Kenya Airways kuelekea Dubai kabla ya kukamatwa na kuhojiwa na Maofisa wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai nchini humo na wachunguzi kutoka Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA).

Sheria za Usimamizi wa Forodha za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za mwaka 2004, Kifungu 85(3) na Kiambatisho cha Pili Sehemu B (4) huharamisha usafirishaji wa madini ambayo hayajapitia viwandani katika kanda ya Afrika Mashariki.

Vipande hivyo vya dhahabu vya uzito wa kilo 32.3 vinashikiliwa na maofisa wa idara ya forodha wa KRA huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

CREDIT: BBC Swahili

Comments

Popular posts from this blog