Mke na Mme Waliokamatwa na Madawa China, Familia Yaanika A-Z

Baraka Malali na mkewe pamoja na mtoto wao.

Sakata la Watanzania wawili ambao ni mke na mume kukamatwa na dawa za kulevya ‘unga’ nchini China na mtoto wao kurudishwa Bongo, limeingia sura mpya, baada ya familia za pande zote mbili kuzungumza na siri ya safari yao kufichuka, Ijumaa Wikienda lina ukweli wa tukio hilo.
Wakazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam, Baraka Malali na mkewe Ashura Musa walikamatwa Januari 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Baiyun jijini Guangzhou, China wakiwa wamemeza jumla ya pipi 129 za dawa za kulevya zilizosadikika kuwa ni heroin. Mume alipakia pipi 47 na mkewe pipi 82.

Taarifa zilieleza kuwa, mamlaka nchini humo ziliamua kumrudisha nyumbani mtoto wao ambaye aliwasili Bongo wikiendi iliyopita kukabidhiwa kwa Ustawi wa Jamii, wakati mipango ya kumkabidhi mtoto huyo kwa ndugu wa wazazi wake ikiendelea.
Baada ya kujiri kwa tukio hilo, Ijumaa Wikienda lilizungumza na wazazi wa watuhumiwa hao na Idara ya Ustawi wa Jamii kujua kwa undani nini kilijiri katika tukio hilo lililoleta simanzi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wanandoa hao.
Mtoto alivyorejeshwa Tanzania.

WIKIENDA KATIKA OFISI ZA USTAWI WA JAMII
Afisa Mwandamizi wa Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam, Derick Lugina alisema kuwa, baada ya kumpokea mtoto huyo, atakabidhiwa kwa babu yake mzaa mama anayejulikana kwa jina la Hashim Musa, mkazi wa Vingunguti, Dar.
“Baada ya wazazi wa mtoto huyo kukamatwa, walitoa maagizo kadhaa, ikiwemo mali zao zilizokuwa kwenye chumba chao walichopanga Magomeni, Dar,” alisema na kuongeza:
“Walisema kuwa vitu vyote vilivyokuwa kwenye chumba hicho apewe mama wa mwanamke anayeishi Vingunguti jijini Dar es Salaam.”
Kuhusu suala la malezi ya mtoto, ofisa huyo alieleza kuwa Idara ya Ustawi wa Jamii inatarajia kutoa uamuzi wa mtu wa kumkabidhi mtoto huyo na tukio hilo la kumkabidhi linatarajiwa kufanyika leo Jumatatu.
“Tunasubiri mkutano wa wazazi hao wa pande mbili; familia ya upande wa baba wa mtoto inayoishi Gairo mkoani Morogoro na familia ya mama. Familia hizo zitakutana na kukubaliana kwanza,” alisema Lugina.
Wazazi hao na mtoto wao.

WAZAZI WA ASHURA WANASEMAJE?
Ijumaa mchana, baba wa Ashura, Hashim alisema kuwa, baada ya kupata taarifa hizo familia ilikuwa katika vikao vya hapa na pale kujadili suala hilo.
“Ukweli nilioambiwa mwanangu ameshakamatwa huko na hapa tuko kwenye kikao cha kujadili suala hilo sasa wewe unataka nini?” Alihoji Mzee Hashim na kuendelea:
“Mimi nina matatizo bwana, hebu niache au nipigie baadaye maana hapa utanichanganya tu.”
Hata hivyo, alipopigiwa baadaye Mzee Hashim aligoma kuzungumzia suala hilo kwa undani akimtaka mwandishi wa habari hii kwenda China kuifuatilia mwenyewe.

BABA WA BARAKA ANASEMAJE?
Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, baba wa Baraka alisema: “Ni kweli mwanangu na mkewe wamepatwa na hayo matatizo na hapa tunavyoongea tuko kwenye kikao cha kujadili hilo suala.”
Aliendelea kueleza: “Mimi nitakuja huko Dar es Salaam kabla ya siku ya Jumatatu kwa ajili ya kuweka sawa baadhi ya mambo wakati tukifuatilia ili kujua hatima yao huko waliko.”

WALIPITIA WAPI?
Habari za ndani zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa, wanandoa hao walisafirisha dawa hizo za kulevya kupitia nchi jirani ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

HUKUMU KUNYONGA YALIZA WENGI?
Sheria za China kuhusu makosa ya dawa za kulevya zimegawanyika. Katika Kisiwa cha Macau, Hong Kong ambako mwanamitindo Mtanzania Jacqueline Patrick ‘Jack Patrick’ alikamatwa ambapo huko adhabu yake kwa kosa hilo ni kifungo.
Lakini kwa upande wa China ya Beijing, wanaopatikana na kosa la dawa za kulevya adhabu yake huwa ni kunyongwa hivyo kuibua vilio kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Kwa mantiki hiyo, ikithibitika walichobeba ni dawa za kulevya, wanandoa hao watakabiliwa na adhabu ya kunyongwa.

Comments

Popular posts from this blog