MGUU WA MTOTO WANASA KWENYE NGAZI ZA UMEME AIRPORT
MTOTO Julian mwenye umri wa miaka miwili alijikuta akivunjwa mifupa ya mguu wake uliponasa kwenye ngazi za umeme katika kiwanja cha ndege cha Vancouver, Canada.
Julian alikuwa na wazazi wake, Andrea Diaczok, mama yake, na baba yake, Jeff Lee walikuwa wakirejea mjini Calgary wiki iliyopita kutokea Vancouver. Mguu wa mtoto huyo ulikwama pembeni kati ya ngazi na vyuma vinavyozungusha mikanda inayopandisha abiria.
“Mguu wake ulipotea kabisa kwenye mkanda unaozunguka,” Diaczok, alisema na kuongeza kwamba kuona hivyo alipiga kelele kwa nguvu.
“Mtambo huo uliukunja mguu wake na kuvunja mifupa ya mguu ambapo kiatu chake kilipotelea ndani ya mkanda huo wenye kuzunguka,” alisema.
Kiatu cha Julian kilikuwa kimebanwa kwenye mkanda huo na ilibidi wafanyakazi wa uwanjani hapo na wapita njia kumng’oa mahali hapo aliponasa.
Diaczok na Lee ambao ni wafanyakazi katika fani ya afya, walikuwa wamejitayarisha kwamba mwanao angekatwa mguu. Hata hivyo, madhara hayakuwa makubwa sana, kwani mbali na mifupa iliyokuwa imevunjika na miteguko kadhaa, madaktari waliweza kuhakikisha mtoto huyo anapata matibabu ambayo hayakuwalazimisha kuukata mguu huo.
Comments
Post a Comment