Kiongozi CHADEMA Auawa, Mbowe Asimulia Alivyotekwa, Mwili Wake Waokotwa Ufukweni

 
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kiongozi wa chama hicho katika Kata ya Hananasif, Daniel John amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Februari 13, 2018, Mbowe alisema John alitoweka siku moja iliyopita. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hana taarifa hizo lakini anawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni.
 
Amesema baada ya mawasiliano atatoa ufafanuzi leo  Februari 14,2018. Mbowe alisema John ambaye ni katibu kata alitoweka akiwa na Reginald Mallya ambaye alijikuta yupo ufukweni mwa bahari.
Mbowe alisema walitoa taarifa polisi kuhusu kutoweka kwa John na kwamba, walipokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) walielezwa kuna mwili ulipelekwa na polisi. Alisema mwili huo ulitambuliwa na mkewe John na una michubuko inayoashiria alikabwa, una jeraha la panga kichwani na upande mmoja wa kichwa umebonyea kuashiria alipigwa na kitu kizito.
Kuhusu Mallya alisema alipigwa panga kichwani na alivunjwa mkono. Mbowe ametaka polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo. Mallya aliyekuwapo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari alisema walikuwa wakitembea na John ndipo waliposimamishwa na kuingizwa ndani ya gari.
Alisema alipigwa hadi kupoteza fahamu na alipozinduka alijikuta ufukweni alikojikokota hadi barabarani ambako alipata msaada wa bajaji na alikwenda Hospitali ya Mwananyamala alikotakiwa kuwa na taarifa ya polisi ambayo aliipata Kituo cha Polisi Oysterbay.

Comments

Popular posts from this blog