Haya ndio mambo matatu waliozungumza Zitto Kabwe na Mh.Lissu Ubelgiji
Jana Jumapili Februari 11, 2018 Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Mhe. Zitto Kabwe alimtembelea Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Mhe Tundu Lissu ambaye yupo kwenye matibabu nchini Ubelgiji.
Zitto Kabwe amesema kuwa walipokutana waligusia mambo makubwa matatu ambayo ni juu ya Gharama za matibabu yake, Suala la uchunguzi wa shambulio lake na maendeleo ya afya yake na mbinu za kuleta mabadiliko nchini.
Kuhusu suala la matibabu Mhe. Zitto Kabwe amesema Lissu anasikitika kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mpaka leo sio tu halimhudumii Lakini pia hata stahili zake za msingi kama Mbunge hapewi. Licha ya kutibiwa kwa misaada ya wasamaria wema, lakini ana mahitaji mengine kama mwanadam na wajibu kama mzazi. Sheria ya Bunge imeweka wazi kuwa Mbunge anapokuwa ametibiwa nje ya nchi Bunge humgharamia maisha yake.
“Suala la Gharama za matibabu yake.,Lissu anasikitika kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mpaka leo sio tu halimhudumii Lakini pia hata stahili zake za msingi kama Mbunge hapewi. Licha ya kutibiwa kwa misaada ya wasamaria wema, lakini ana mahitaji mengine kama mwanadam na wajibu kama mzazi. Sheria ya Bunge imeweka wazi kuwa Mbunge anapokuwa ametibiwa nje ya nchi Bunge humgharamia maisha yake.
Tangu Septemba, 2017 Bunge halijampa Mbunge wa Singida Mashariki haki zake za kisheria. Bunge limesukuma wajibu huo kwa Serikali, Wizara ya Afya na linasema kuwa linasubiri urasimu wa Serikali. Inasikitisha sana. Ikumbukwe kuwa mmoja wa wataalamu waliosaidia Lissu kupata huduma ya kuokoa maisha yake katika Hospitali ya Mkoa ya Dodoma, mara tu baada ya kupigwa risasi, ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
Mzunguko ambao unafanywa na Bunge kuhusu suala lililo wazi kabisa la kugharamia maisha ya Mbunge aliye kwenye matibabu linatia simanzi sana. Ninamsihi Spika wa Bunge, achukue hatua kwenye jambo hili, Bunge litimize wajibu wake kwa Mbunge wake kwa mujibu wa sheria. Kuendelea kuvuta miguu katika suala hili kunaleta hisia mbaya, na kunajenga taswira mbaya ya Bunge letu.“ameeleza Mhe. Zitto Kabwe kwenye taarifa yake kwa Vyombo vya Habari.
Akielezea mambo mengine waliyonena na Mwanasheria Lissu, Mhe. Zitto Kabwe amesema waligusia pia kuhusu kucheleweshwa kwa hatua za kiuchunguzi wa tukio la kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mnamo mwaka Septemba 7, 2017. Ambapo Lissu amewataka Watanzania waendelee kupaza sauti ili uchunguzi ufanyike na kuwakamata wahusika waliomshambulia.
“Suala la uchunguzi wa shambulio lake. Mpaka sasa ni miezi mitano imepita tangu Lissu ashambuliwe kwa risasi, na hakuna taarifa yeyote kuwa mamlaka za uchunguzi zimewakamata wahusika au kuonyesha tu juhudi za kuwatafuta wahusika. Jambo hili linatoa taswira mbaya sana juu ya vyombo vyetu vya uchunguzi, linajenga chuki na linaondoa imani ya wananchi kwa vyombo hivyo.
Ombi la Lissu kwangu ni kuwa tuendelee kupaza sauti ili uchunguzi ufanyike na kuwakamata wahusika waliomshambulia. Iwapo watu hawa hawatachukuliwa hatua wataendelea kuumiza watu wengine. Jeshi la Polisi linapaswa kueleza umma limekwama wapi kwenye uchunguzi wa tukio hili baya kabisa kuwahi kutokea katika nchi yetu, la mbunge kushambuliwa kwa risasi katika eneo la Bunge, akihudhuria vikao vya bunge.
Ni jambo la aibu kubwa kwa nchi yetu kuwa Mbunge anashambuliwa mchana kweupe na vyombo vya uchunguzi vinashindwa kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuwakamata wahusika. Kitendo cha Serikali kukataa kuchunguza shambulio hili ni ishara kuwa Serikali inawajua waliomshambulia Lissu, na hivyo imeamua kuwalinda. Jambo hili ni baya sana kwa ustawi wa haki katika nchi yetu.“ameeleza Zitto Kabwe.
Jambo lingine walilozungumzia ni kuhusu mbinu za kuleta mabadiliko nchini ambapo Zitto amesema ameambiwa na Mhe. Lissu kuwa Watanzania wapo tayari kwa mabadiliko ila kikwazo ni viongozi tu.
“Tulibadilishana mawazo na juu ya mbinu za mapambano ya kuleta mabadiliko nchini kwetu. Lissu ameniambia maneno yafuatayo “Wananchi wanajua wanataka nini, sisi Viongozi ndio tupo nyuma na Wananchi wapo mbele kimawazo. Jambo moja lipo wazi sana kwangu nalo ni kuwa sikati tamaa na Watanzania“amemaliza kwa kunukuu Zitto Kabwe.
Mnamo Januari 6, 2018 Mhe. Tundu Lissu alipelekwa nchini Ubelgiji akitokea Kenya alikokuwa anapatiwa matibabu hapo awali kwa ajili ya matibabu zaidi.
Comments
Post a Comment