Hatma ya Zitto mikononi mwa Spika

KUADHIBIWA ama kutoadhibiwa na Bunge kwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) kuko chini ya Spika Job Ndugai baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kukamilisha uchunguzi wa shauri lake.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo anakabiliwa na tuhuma za kudharau mamlaka ya Spika kutokana na kauli yake kwamba, "Bunge limewekwa mfukoni na serikali."

Akiwasilisha bungeni mjini hapa jana taarifa ya shughuli za Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kipindi cha kuanzia Januari 2017 hadi Januari 2018, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Almas Maige, alisema tayari wameshakamilisha uchunguzi wa shauri hilo.

Pia alisema kamati yake imeshamshauri Spika hatua za kuchukua kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016.

Maige ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), alisema kuwa katika mkutano wa nane wa Bunge, baada ya Spika kupokea na kuikabidhi serikali taarifa za kamati mbili alizoziunda Julai tano kwa ajili ya kufanya uchunguzi katika sekta ya madini, Zitto aliandika kwenye mtandao wa Twitter maneno ya dharau dhidi ya Spika.

Spika aliunda kamati mbili za kuchunguza na kuishauri serikali kuhusu mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya madini ya Tanzanite na almasi.

"Kamati ilifanya uchunguzi wa shauri hili na kukamilisha kisha kumshauri Spika kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge," Maige alisema.

Spika Ndugai hakuongoza kikao hata kimoja katika mkutano wa wiki mbili uliomalizika jana.

Comments

Popular posts from this blog