Waziri Mpina awasilisha majina ya Viongozi waliokaidi agizo la Serikali


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewasilisha majina ya viongozi wa halmashauri ambazo hazijaanza kutekeleza upigaji chapa mifugo na zile ambazo ziko chini ya asilimia 10 ya utekelezaji,

Kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo ili zichukuliwe hatua.

Mpina alibainisha hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa upigaji chapa mifugo nchini, mjini Dodoma.

Alisema kwa tathmini iliyofanyika hadi sasa jumla ya ng’ombe 10,306,359 sawa na asilimia 59.3 wamepigwa chapa huku asilimia 40.7 wakiwa hawajapigwa chapa na zoezi hilo linatarajiwa kukamilishwa Januari 31, mwaka huu.

“Halmashauri 100 zimepiga chapa zaidi ya asilimia 50, halmashauri 54 zimepiga kati ya asilimia 10 hadi 50, halmashauri 14 zimepiga chini ya asilimia 10 na Halmashauri 9 hazijaanza kupiga chapa,” alisema Mpina.

Alizitaja halmashauri ambazo hazijaanza kabisa ni Tandahimba, Nanyumbu, Mafia, Newala, miji ya Newala, Nanyamba na Masasi na manispaa za Kigamboni na Ilemela.

Kwa upande wa punda, Mpina alisema jumla ya punda ni 572,353 na watapigwa chapa.

Alibainisha kuwa sababu za kutokamilika kwa zoezi ni uwapo wa changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wafugaji kukataliwa kupigiwa chapa mifugo yao kwa kisingizio kuwa ni wavamizi au wahamiaji haramu.

“Mfano katika wilaya za Kibiti, morogoro, Rufiji, Sumbawanga, Tanganyika na Kibondo wamekumbana na changamoto hii,”alisema Mpina

Aidha alitaja changamoto nyingine kuwa ni wafugaji kuhamisha ng’ombe katika kipindi hichi cha kilimo na hivyo kutoshiriki, baadhi ya ng’ombe kuendelea kuwa katika maeneo ya hifadhi na Mapori Tengefu mfano kwa mkoa wa Kigoma na Ruvuma.

“Pia baadhi ya wafugaji kuendelea kugoma kupiga chapa mifugo yao kutokana na imani potofu na wengine kuficha idadi ya mifugo kwa mfano mkoa wa Manyara,”alisema

Mpina alisema kuwakatalia wafugaji kupiga chapa kwa kisingizio cha uhamiaji haramu haikubaliki kwa kuwa wilaya zote zilipewa jukumu la kuhakiki mifugo yao na kuwasilisha taarifa Wizarani.

“Hakuna halmashauri hata moja iliyoleta taarifa za wahamiaji haramu, pia zoezi lisihusishwe na migogoro ya muda mrefu ya matumizi ya ardhi, mifugo yote ipigwe chapa isipokuwa ile ya kutoka nchi jirani,”alisema

Kadhalika, Mpina alisema wafugaji watakaoshindwa kufanya hivyo ndani ya muda uliowekwa hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji namba 12 ya mwaka 2010 ibara ya 4 kifungu cha 26.

Comments

Popular posts from this blog