Rais Magufuli ammwagia sifa Kagame

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amefunguka na kusema kuwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame atalisaidia bara la Afrika kusonga mbele kimaendeleo kwa kuwa kiongozi huyo anajua matatizo na shida za nchi nyingi za Afrika.

Magufuli amesema hayo leo Januari 14, 2018 akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mazungumzo yake na Rais Kagame ambayo yamefanyika leo Ikulu na kusema kuwa Kagame ni mwanamapinduzi wa kweli wa Afrika hivyo atakavyokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika atalisaidia bara hilo kusonga mbele zaidi.

"Kagame atakapokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) sisi Tanzania tumeipokea hii kwa raha sana kwa sababu tunamfahamu Rais Kagame lakini pia ni jirani yetu mwema sasa Mwenyekiti atakuwa anatoka ndani ya East Africa Community, nimemuakikishia kuwa sisi Tanzania tutampa ushirikiano wa hali ya juu sana katika nafasi hii atakayokwenda kuichukua na nimemthibitishia kutokana na ushawishi wake Afrika hivyo atashinda kwa kura nyingi sana" alisema Rais Magufuli

Rais Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa Kagame akichukua nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ataweza kuwakilisha vizuri zaidi na kuleta suluhu katika mambo mengi yanayolikumbuka bara la Afrika.

"Nina uhakika Kagame akishakuwa Mwenyekiti ataweza kuwakilisha vizuri mambo haya, migogoro, ukoloni mambo leo unaoweza kujengwa na mtu yoyote kutoka nje ya Afrika na kuleta matatizo kwa waafrika. Kagame anaufahamu ukweli, Kagame anaufahamu shida za wananchi wa Rwanda, anaijua historia ya Rwanda, anafahamu mateso ya wanyarwanda, uzoefu wake ni mkubwa ndiyo maana mimi naamini kwa mchango wake mkubwa katika Afrika na kwa kuwa mwanamapinduzi mzuri wa Afrika na kwa sababu anawapenda vijana wa Afrika uzoefu huo utasaidia kwenda mbele kwa ajili ya maendeleo ya nchi za Afrika" alisisitiza Magufuli

Mbali na hilo Rais Magufuli na Rais Kagame wamekubaliana katika masuala ya kibiashara kwa kutengeneza mazingira mazuri ya biashara kati ya nchi hizo mbili kwa kujenga Reli ya Standard gauge ambayo itakwenda mpaka Rwanda.

Comments

Popular posts from this blog