Kigwangala atoa siku saba kwa Kampuni za Uwindaji Nchini
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala, ametoa siku saba kwa kampuni sita za uwindaji nchini kufika katika ofisi za wizara hiyo Dodoma, kujieleza kutokana na tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Dk. Kigwangala alisema kampuni hizo zina leseni halali za uwindaji, lakini ndani yake wamekuwa wakifanya vitendo ambavyo vinaashiria uvunjifu wa sheria na uhalifu dhidi ya wanyama.
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Berlette Safari Corporation Ltd, Game Frontiers of Tanzania Ltd, Mkwawa Hunting Safaris Ltd, Tanzania Game Trackers Safaris Ltd, Wengert Windrose Safari Ltd na Geenniles Safaris Ltd.
Alisema wakurugenzi wa kampuni hizo na washirika wao wanatakiwa kufika ofisi za Wizara Dodoma kuhojiwa na kikosi kazi maalum kuhusiana na tuhuma hizo.
“Waje hapa wazungumze na kikosi hiki wajieleze ni kwa nini tusichukue hatua za kisheria dhidi yao, lakini pia wajibu hoja mbalimbali zitakazohusisha makosa mbalimbali. Wakurugenzi wote na washirika wao wafike wao wenyewe bila kutuma uwakilishi na bila kutoa sababu zozote,” alisema.
Alisema baada ya kuwahoji watachukua hatua za kiutawala kulingana na sheria ya uwindaji na baada ya hapo kwa makosa yatakayojulikana ni ya jinai yatapelekwa vyombo vya dola vinavyohusika na makosa hayo ikiwamo ya ujangili kama itabainika kwenye kikosi hicho.
Dk. Kigwangala alitaja tuhuma zingine kuwa ni uwindaji haramu, uhawilishaji wa umiliki wa vitalu vya uwindaji bila kufuata sheria, ikiwamo makosa ya ujangili, kujaza fomu za udanganyifu, rushwa, uhalifu dhidi ya rasilimali za wanyamapori, uhujumu uchumi, ukiukwaji wa kanuni za uwindaji na kutolipa tozo mbalimbali.
Pamoja na kampuni hizo, alimwagiza mmoja wa watumishi wa wizara hiyo, Alex Aguma, afike pia kuhojiwa.
MTANDAO WA MAJANGILI
Waziri huyo alisema katika kipindi cha siku 100 ambazo amekuwa katika nafasi hiyo, wizara hiyo imekamata watuhumiwa 74 na kubaini mitandao yao yote na hatimaye kubainisha mtandao mzima ambao una washirika 949 wa ujangili.
Alisema kati ya hao nusu wamechukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani na kwamba wanaendelea na ufuatiliaji wa watuhumiwa wengine ambao wametajwa na washiriki wao, lakini wengine wamekimbia maeneo mbalimbali.
“Lakini pia napenda kutambua kazi kubwa iliyofanywa tangu mwaka 2010 hadi 2013-2014 ambao ilikuwa mwisho wa operesheni tokomeza ambayo ilikuwa inajibu mashambulizi kutokana na kukithiri kwa ujangili ambao ulikuwepo mwaka 2010-2015.
“Operesheni tokomeza serikali iliweza kubainisha watuhumiwa mbalimbali takribani 2130 ambao walituhumiwa kwa uhujumu uchumi, lakini kukutwa kwa silaha 3715 zilizokamatwa, meno ya tembo ghafi 3789 yenye uzito wa kilo 12,194, vipande 695 vya meno yaliyochakatwa,”alisema.
Jangili adakwa Loliondo
Aidha Dk.Kigwangala alisema usiku wa kuamkia jana amekamatwa muuaji Loliondo ambaye yeye kazi yake ni kulenga shabaha na silaha anachukua kwa mtu mwingine.
“Tumetengeneza utaratibu wa kuwafuatilia katika ngazi tofauti tofauti hadi tuvunje mtandao mzima wa ujangili hapa nchini, na sasa tunawatambua kwa ngazi tano za ujangili na biashara haramu na tunawabainisha majangili kwa madaraja yao, daraja la anayeenda kuua, kulenga shabaha, kusafirisha, wakala, anayefadhili, anayevuka mipaka kwenda nchi nyingine, mitandao ya kuuza nyara nje ya nchi,” alisema.
Comments
Post a Comment