DC aamuru mkandarasi akamatwe

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, John Palingo ameamuru kuwekwa mahabusu mkandarasi wa umeme kutoka Kampuni ya Cyber, Benjamin John baada ya kutuhumiwa kuchukua fedha kwa wananchi kwa madai ya kuwaunganishia umeme wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) katika vijiji ambavyo havipo kwenye mpango huo.

Palingo alitoa amri hiyo jana kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mbozi baada ya baadhi ya madiwani kudai kampuni hiyo imekuwa ikiwatoza baadhi ya wananchi Sh20,000 hadi 140,000 kwa ajili ya fomu na usajili wa mteja kuunganishiwa umeme.

Kutokana na malalamiko hayo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Erick Ambakisye alilazimika kuuita uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Songwe na mwakilishi wa Kampuni ya Cyber kutoa ufafanuzi mbele ya baraza hilo.

Hata hivyo, Mkandarasi na mwakilishi wa Kampuni ya Cyber, Benjamini John alipotakiwa kutoa ufafanuzi alikanusha madai hayo akieleza kwamba iwapo itathibitika kuwa kampuni yake imehusika, fedha hizo zitarejeshwa kwa waliotapeliwa.

“Hizi ni tuhuma, naamini vyombo vya dola vitachunguza na mwisho wa siku ukweli utabainika, hata hivyo kampuni hii imesajiliwa kihalali lakini pia kutokana na ushindani wa kibiashara inawezekana miongoni mwa madiwani ni washindani wetu wametuingiza katika kashifa hii,” alisema John.

Akitoa uamuzi wake, Mkuu wa wilaya hiyo Palingo aliamuru polisi kumshikilia mkandarasi huyo kwa ajili ya uchunguzi na kuwataka madiwani kwa upande wao kuwasilisha ushahidi wa tuhuma wanazodai ofisini kwake ifikapo Jumatatu ili hatua zaidi zichukuliwe

Comments

Popular posts from this blog