SPIKA NDUGAI AIKOSOA SERIKALI UPANGAJI WA VITUO VYA KAZI KWA WALIMU WAPYA
DODOMA: Spika wa Bunge, Job Ndugai amekosoa mpango wa TAMISEMI kuwapangia walimu wapya vituo vya kazi moja kwa moja akisema kazi hiyo ni ya Halmashauri kwani ndizo zinazofahamu maeneo yenye uhaba wa walimu.
Ndugai amesema hayo leo Jumamosi Desemba 23,2017 ikiwa ni siku moja baada Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo kutangaza majina ya walimu wapya 3,033 waliopangiwa vituo vya kazi. Katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Dodoma, Ndugai amehoji Tamisemi ni nani hata aweze kujua ikama ya walimu shuleni. Amesema wamekuwa wakijaza walimu maeneo yasiyo na mahitaji na kuyaach maeneo yenye uhitaji.
“Jambo hili linakera, kila mahali sasa ni Tamisemi hadi napata shaka, hivi hii zana ya D by D (ugatuaji wa madaraka) ina maana haijatafsiriwa vyema au ndiyo kupoka madaraka kwa wengine?” alihoji Ndugai.
Akitoa mfano wa Shule ya Banyibanyi wilayani Kongwa, Ndugai alisema ina wanafunzi wanaoingia kidato cha tatu lakini hawajawahi kusoma masomo ya sayansi hata siku moja.
“Juzi mmepanga walimu na nilipita tena hapo hakuna hata mwalimu. Hawajasoma hesabu, fizikia, baiolojia, kemia na jiografia; nauliza tena wanasema Tamisemi, hivi hao walisoma wapi na ninyi mmesoma shule zipi?” alihoji na kuwasihi wabunge wa Mkoa wa Dodoma kuwa wanatakiwa kuupinga mpango huo bungeni wakati yeye akiongoza vikao vya Bunge.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge amewaagiza wakurugenzi wote wa wilaya kuangalia ikama ya walimu na kuwatawanya vituoni mara moja.
Comments
Post a Comment