Waziri Wa Tamisemi Atoa Maagizo 6 Kwa Wakuu Wa Mikoa


Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo.
Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, ametoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kufuatia kutangazwa kwa matokeo ya darasa la saba.
Waziri Jafo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo, ameeleza kwamba jumla ya watahiniwa 909,950 walifanya mtihani ambapo watahiniwa 662,035 wamefauli kwa daraja A – C ikiwa ni sawa na 72.76% ya watahiniwa wote.
Kufuatia ufaulu mkubwa uliojitokeza ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikalli za Mitaa, imetoa maelekezo kwa mikoa yote ili waweze kuanza maandalizi mapema ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mapema mwakani kabla ya kukamilika kwa uchaguzi wa wanafunzi hao.
Ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu mitihani wanapata nafasi ya kujiunga kidato cha kwanza Januari 2018, maelekezo yafuatayo yametolewa.
1. Wakuu wa Mikoa yote wametakiwa kuhakikisha kuwa miundombinu iliyopo inatosha katika mikoa yao ili wanafunzi waliofaulu wapate nafasi ya kujiunga kidato cha kwanza Januari 2018.
Mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Kagera, Njombe, Tanga, Morogoro, Lindi, Rukwa, Pwani, Mtwara na Songwe imetakiwa kufanya maandalizi ya kutosha ya vyumba vya madarasa, madawati na vyoo kwani kiwango cha ufaulu katika mikoa hiyo kimeongezeka.
2. Makatibu Tawalawa Mikoa wametakiwa kusimamia zoezi la uchaguzi wa wanafunzi waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza na kufikia Novemba 30, mwaka huu zoezi hilo liwe limekamilika.
Ngazi ya kitaifa, Wizara itatangaza matokeo ya uchaguzi Disemba 7, 2017 hivyo mikoa yote itatakiwa itangaze matokeo hayo Disemba 8, 2017 ili kuwapa wazazi muda mzuri wa kufanya maandalizi ya wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza.
3. Makatibu Tawala wa Mikoa wametakiwa kuhakikisha kuwa wanaandaa utaratibu mzuri utakaosaidia kuimarisha ujifunzaji wa somo la Kiingereza katika shule za msingi kwani ufaulu wake umeshuka sana.
4. Mikoa ambayo watahiniwa zaidi ya 1% hawajafanya mitihani, wafanye uchunguzi wa kina ili kubaini sababu za hali hiyo na kuandaa mikakati ya kuiondoa.
Mikoa iliyotajwa ni pamoja na Geita, Katavi, Mara, Rukwa, Mbeya, Songwe, Dodoma na Manyara.
5. Halmashauri za Mkarama, Meatu na Simanjiro zilizopata wastani wa chini 50% katika kiwango cha ufaulu zijipange kikamilifu kupandisha ufaulu wa wanafunzi katika masomo na kupanga mikakakti shirikishi ili hali hiyo isijirudie tena.
6. Viongozi wa serikali za Mikoa na Mamlaka za serikali za Mitaa zimetakiwa kujipanga upya kusimamia kuongeza juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuboresha elimu nchini kwa kushirikiana na wadau wengine.
Waziri Jafo ameeleza kuwa, kufuatia maelekezo hayo wizara haitarajii kusikia kuna wanafunzi walioshindwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa sababu yoyote ile, hivyo wahusika wahakikishe kuwa wanafanya juhudi ili kukamilisha maagizo hayo.

Comments

Popular posts from this blog