Vurugu Zatanda Kenyatta Akiapishwa, Polisi Wafunga Mtaa Kuzuia Mkutano wa NASA
MTAA wa Jacaranda jijini Nairobi, Kenya, leo umefungwa na polisi ili kuzuia mkutano wa umoja wa vyama vya upinzani nchini humo, National Super Alliance (NASA) uliopangwa kwa ajili ya kuwakumbuka wafuasi wake 27 waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga uchaguzi wa marudio uliofanyika zaidi ya wiki moja iliyopita.
Mkutano huo ulipangwa kufanyika leo ambapo Rais Uhuru Kenyatta ameapishwa kwa kipindi cha pili katika uwanja wa michezo wa Kasarani. Chumba vya kutunzia maiti katika jiji hilo pia kimefungwa na polisi ambapo watu hawatakiwi kufika hapo.
Polisi waliokuwa na zana zote za kuzuia fujo wamekuwa wakirusha mabomu ya machozi sehemu nyingi yakiwemo maeneo ya wafuasi wa NASA ambao wamefunga barabara kadhaa jijini humo.
Mpinzani mkuu nchini humo, Raila Odinga, amepinga mipango ya kumwapisha katika nafasi ya urais, akisema hilo linaweza kuleta vurugu na vifo zaidi.
Aliyasema hayo akionyesha mifano ya nchi za Ivory Coast na Gambia ambazo zilifanya hivyo kutokana na migogoro ya uchaguzi na hivyo kuwaapisha Alassane Quatara na Adama Barrow, hali aliyosema si sawa na ile iliyotokea nchini Kenya.
Pamoja na kuzuiwa kwa mkutano huo wa upinzani, inasemekana polisi wamepiga kambi karibu na makazi ya viongozi wa NASA, akiwemo Mbunge wa Dagoretti Kaskazini, Simba Arati.
Comments
Post a Comment