Rais Magufuli Anastahili Pongezi, Amefunua Blanketi Lililotufunika
MUNGU ni mwema kwa sababu ametufikisha leo tukiwa wazima, hakika ahimidiwe daima.
Leo nachukua nafasi hii kumpongeza Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa mafanikio aliyotuletea ndani ya miaka miwili ya utawala wake.
Ninapofanya tathmini ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Magufuli, ni kama narudia kwa sababu juzi na jana wengine wameandika au kusema kupitia vyombo vya habari.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015 na Rais Magufuli kuibuka mshindi, alianza kuonesha kwa haraka kuwa yeye ni kiongozi asiyetaka mchezo kwenye kazi.
Aliliambia taifa kuwa alipokea nchi ikiwa imejaa uozo kila idara na alitumia hoja hiyo kukataa hoja ya kupendekezwa kwa Katiba Mpya, iliyowahi kutolewa na baadhi ya watu wakati alipotimiza mwaka mmoja madarakani kwa kusema wazi, ‘niacheni niisafishe nchi kwanza.’
Mwaka wake wa kwanza alifanya mengi yaliyowafurahisha wananchi wengi, kama vile kufuta safari za nje kwa maofisa wa serikali labda kama ni za lazima sana na kibali cha kwenda huko kutolewa na ofisi yake.
Lakini pia alifurahisha watu alipotembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kujionea wagonjwa walivyokuwa wakitaabika kwa kulala sakafuni, akaamua kupeleka vitanda vya wagonjwa.
Kama ilivyo desturi, kwenye mazuri hapakosi wapinzani, baadhi ya watu wakadhani kwamba hiyo ilikuwa ni nguvu ya soda, lakini kadiri siku zilivyokwenda, hajaonesha dalili zozote za kurudi nyuma.
Lakini jambo kubwa pengine kuliko yote aliyoyafanya, ni kuonesha jinsi nchi hii ilivyokuwa ikiibiwa madini yetu na watu wa nje kwa kushirikiana na Watanzania wachache ambao kwangu mimi nawaona kuwa walikosa uzalendo.
Uamuzi wake mkubwa wa kusimamia marekebisho ya sheria ambayo itaifanya nchi inufaike na rasilimali zake, hususan madini, ndiyo uthibitisho kuwa kiongozi wetu huyu bado hajaonesha dalili za kurudi nyuma katika kupigania maslahi ya nchi kwa faida ya watu wote bila kujali itikadi zetu.
Hiyo ni pamoja na hatua ya serikali yake kuingia mkataba upya na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick ambayo sasa itagawana faida yake nusu kwa nusu na serikali.
Barrick pia ilikubali kutoa hisa zake asilimia 16 katika kila mgodi wake kwa serikali na kutoa shilingi bilioni 700 kuonesha nia njema ya kuendelea na mazungumzo ya kujadili kulipa fidia ya mapato ambayo serikali ilikuwa ikipoteza kwa miaka zaidi ya 15 kutokana na kampuni hiyo kufanya udanganyifu wa mapato ya mauzo ya mchanga wa madini maarufu kama makinikia.
Lakini Rais Magufuli aligundua wizi mwingine mkubwa uliokuwa ukifanywa na watu wasio waaminifu baada ya kubaini kuwa kuna wafanyakazi hewa wa serikali.
Zoezi hilo lilifanyika na akaokoa mamilioni ya fedha ambazo zilikuwa zikienda kwenye mifuko ya watu binafsi ambao walikuwa wakinufaika na fedha hizo za umma.
Aliona pia kuwa kuna tatizo la watumishi wa serikali ambao walikuwa wakitumia vyeti feki na akarudisha nidhamu katika utumishi wa umma.
Ndani ya miaka hiyo miwili alidhibiti wizi bandarini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hivyo kuliingizia taifa matrilioni ya shilingi ambazo huko nyuma zilikuwa zikinufaisha wachache.
Ndugu zangu, wengi tunajua jinsi Shirika la Ndege Tanzania (ATC), lilivyoporomoshwa na wenzetu waliopewa dhamana kuliendesha, baada ya kuingia madarakani Rais Magufuli, serikali yake imeweza kununua ndege mpya ndani ya muda mfupi na hivi sasa zinafanya kazi.
Serikali yake ilifuta shamrashamra za sherehe za kitaifa na badala yake fedha ambazo zingetumika kwenye sherehe hizo akazielekeza kwenye miradi ya barabara Dar es Salaam na Mwanza.
Hakika aliyoyafanya mazuri kwa taifa letu ni mengi na hii imetufanya Watanzania tulio wengi kuona kama vile ametufunua kwenye blanketi kwani wengi kasoro hizo walikuwa hazioni.
Hata hivyo, kuna kasoro ambazo baadhi ya watu wanaikosoa serikali kama vile kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya kisiasa kwa viongozi wa vyama hadi mwaka 2020. Hata hivyo, wabunge kwenye maeneo yao wameruhusiwa kuzungumza na wapiga kura wao.
Lakini pia wapo wanaoona kwamba suala la Katiba Mpya serikali isiliweke kapuni kwa sababu tayari mabilioni ya shilingi za walipa kodi zimeshatumika.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Comments
Post a Comment