Polisi wamnasa muuza risasi za kivita

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam linawashikilia watu wawili kwa mahojiano baada ya kukamatwa na risasi za kivita ambazo wanazimiliki kinyume na sheria.

Akitoa taarifa kwa Wanahabari Kamanda Mambosasa amesema kwamba Novemba 6 mwaka huu maeneo ya Serengeti Kigamboni lilipokea taarifa ya kuwepo kwa mtu mmoja anayefahamika kwa jina la Willy Peter kuwa anafanya biashara ya kuuza risasi mtaani.

Amesema kwamba baada ya kupata taarifa hizo Polisi walifanya ufuatiliaji na hatimaye kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na risasi 69 za kivita aina ya FN G3.

Kamanda Mambosasa amefafanua kwamba baada ya  mahojiano mtuhumiwa huyo alikiri kuwa risasi hizo alipewa na mtu aliyemtaja kwa jina la Matabu William kwaajili ya kwenda kuziuza na kwamba alimpatia risasi hizo huko nyumbani kwake Kiwalani jijini Dar es salaam.

Hata hivyo polisi walifika nyumbani kwa Matabu William Matoke (52) kiwalani ambapo alikiri kufanya biashara hiyo ya risasi na alipopekuliwa katika nyumba yake hiyo alikutwa na risasi moja aliyokuwa ameifukia pembezoni mwa nyumba yake na kufanya jumla ya risasi zilizokamatwa kuwa 70.

Imeelezwa kwamba watuhumiwa hao wapo katika mahojiano na baada ya hapo watu hao watafikishwa kwenye vyombo vya sheria

Comments

Popular posts from this blog