Masharti Mapya Mnada wa Nyumba za Lugumi Kesho

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya udalali ya Yono, Scolastica Kevela.
ILI kuhakikisha mnada wa nyumba mbili za Lugumi huko JKT Mbweni na Upanga jijini Dar es Salaam unakwenda vizuri, watu watakaofika na kushiriki mnada huo kesho, watabidi kutimiza masharti kadhaa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya udalali ya Yono, Scolastica Kevela, wote watakaofika maeneo hayo watabidi kutoa vitambulisho vyao vya kazini, vya udereva na vya upigaji kura.

Isitoshe, kwa mujibu wa Kevela, wote watakaoingia mnadani hapo  itabidi watoe Sh. Milioni mbili kama uhakikisho wao wa dhamira ya kushiriki  na kununua  mali husika, hii ikiwa kwa washangiliaji na watazamaji.

Kevela alisema wale watakaoshinda mnada huo, Sh.milioni mbili walizotoa zitakuwa sehemu ya malipo yao, na kwa wale watakaoshindwa, watarudishiwa fedha hiyo baada ya mnada.

Alisisitiza pia kwamba washindi wa mnada huo watatakiwa kulipa asilimia 25 ya bei ya nyumba husika waliyoshinda na asilimia 75 iliyobaki itabidi ilipwe ndani ya siku 14 ambapo atakayeshindwa kufanya hivyo hatarudishiwa fedha iliyotangulizwa ya asilimia 25.

Pia alionya kwamba watu wasiohusika kwa lolote na mnada huo kwamba ni vyema wasifike maeneo hayo ili kukwepa kupambana na sheria pindi wakijikita katika kuharibu mchakato wa mnada huo.
STORI: WALUSANGA NDAKI – GLOBAL PUBLISHERS

Comments

Popular posts from this blog