FAMILIA YA NDIKUMANA YAZUIA IRENE UWOYA ASIPIGWE RWANDA


FAMILIA ya aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Timu ya Rayon Sports ya Rwanda, Hamad Ndikumana ‘Katauti’ (39), imezuia staa wa filamu Bongo, Irene Uwoya ambaye alikuwa mke wa jamaa huyo asifanyiwe fujo baada ya kutinga nchini Rwanda jioni ya Ijumaa iliyopita. Hatua hiyo ilikuja baada ya Ndikumana kupoteza maisha huku Uwoya akishushiwa tuhuma za hapa na pale na kwamba huenda alichangia kifo hicho. Hamad Ndikumana ‘Katauti’ (39) enzi za uhai wake akiwa na staa wa filamu Bongo, Irene Uwoya. Kwa mujibu wa chanzo chetu kilichoambatana na Uwoya, familia ya Ndikumana ilichukua uamuzi huo baada ya watu mbalimbali nchini humo kuwa na hasira na Uwoya.

         Kutokana na kifo cha Ndikumana, Uwoya alilazimika kwenda Rwanda kuhani msiba akiwa na mwanaye aliyezaa na jamaa huyo, Krish, mama na baba yake na mabaunsa wa kumpa ulinzi. Chanzo hicho kilieleza kwamba, watu mbalimbali nchini humo walikuwa na hasira juu ya Uwoya kwamba ndiye aliyesababisha kifo cha Ndikumana kwani alikuwa na msongo wa mawazo akimfikiria yeye kwa kuwa alimpenda na kutaka wairudishe ndoa yao, lakini mwanamama huyo akawa anang’ang’ania apewe talaka ambayo hadi Ndikumana anafariki dunia alikuwa hajaitoa. Staa wa filamu Bongo, Irene Uwoya. “Mashabiki wa Ndikumana walitaka kumfanyia fujo Uwoya kwa kuwa wanadai ndiye chanzo cha kifo cha mpendwa wao, lakini familia iliwazuia wasifanye hivyo kwa kuwa walishamsamehe Uwoya ndipo hali ya amani ikawepo,” kilisema chanzo hicho.

Kiliendelea kueleza kuwa, Uwoya aliwasili nchini Rwanda Ijumaa iliyopita kwenda kuona kaburi la mumewe ambaye alizikwa Jumatano iliyopita ambapo alipokelewa vizuri na mama wa Ndikumana pamoja na familia kwa jumla. “Zile tofauti waliziweka pembeni na mama Ndikumana akamwambia wamemsamehe hivyo ikawa ni kuomboleza upya kwani Uwoya na mama’ke alikuwa akilia sana hadi kushindwa kutembea,” kilisema chanzo hicho. Hata hivyo, alisaidiwa kwa kushikwa mkono na wenyeji kwani mama huyo alikuwa akimpenda sana mkwewe Ndikumana kama mtoto wake.

Baada ya chanzo kutiririka, Ijumaa Wikienda lilimtafuta Uwoya ambaye alikiri kupokelewa vizuri na familia pamoja na mama Ndiku ambaye alipomuona tu alimkumbatia huku akilia kwa uchungu akimuita ‘mwanangu’. Naye msanii wa filamu, Michael Sangu ‘Mike’ ambaye ni mmoja wa watu waliosafiri alikiri kuwa walipokelewa vizuri na hakuna tofauti yoyote iliyojitokeza. “Uwoya, baba, mama na Krish walitangulia na ndege na walipokelewa vizuri kabisa na hakuna mtu aliyewafanyia fujo wala nini, familia imewapokea kwa ukarimu na sisi ambao tulifika baadaye maana tulisafiri kwa basi tulipokelewa vizuri sana,” alisema Mike Sangu.
CREDIT: GPL

Comments

Popular posts from this blog