BONGO MOVIE NIAJE, WALIMSUSA LULU AU?

KUNA mambo katika maisha siyo kanuni, lakini utamaduni umeyafanya kuwa kama ndiyo utaratibu. Na haya yako mengi kutegemea na mila za kila jamii. Huwezi kushtakiwa kwa kutokufanya, lakini wanaojumuika na wewe watakesha wakikushangaa.
Jirani yako akipatwa na matatizo, siyo lazima ujitoe na kumsaidia kwa wakati huo, lakini utamaduni wetu unakuona mtu wa ajabu kama ikikutokea hivyo, halafu wewe badala ya kujumuika naye kwa kumfariji, unaalika watu wa ngoma na kufurahi pamoja nao. Hali iko hivyo kwa wafanyakazi wa ofisi moja, wa tasnia moja na hata watu wanaotoka jamii moja.Kwa mfano, watu wa makabila tofauti kutoka mikoa mbalimbali, wanapokutana katika mkoa au wilaya moja huwa kama ndugu na mmoja wao anapopatwa na matatizo au kuwa na shughuli, wengi hutazamiwa kuwepo.

Katika eneo kama hilo, ingawa huwezi kumpeleka mtu kortini, lakini inapotokea mmoja anashindwa kuhudhuria shughuli hiyo, huonekana kama msaliti kwa wenzake, kitu ambacho kistaarabu kinatia doa. Na kushiriki shughuli ya mtu wa kazini, jamii moja au tasnia moja, haimaanishi kutoa kitu, kwa mfano fedha au kitu chochote, bali ni ile hali ya kuonyesha kuguswa na tukio lililotokea na kibinadamu, kutoa neno la faraja katika mjumuiko huo. Ninasema hivyo baada ya kuguswa na jinsi hali ilivyokwenda kwa msanii mwenye umri mdogo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye kwa muda mwingi wa usikilizaji wa kesi yake ya kuua bila kukusudia, alikuwa akienda mahakamani peke yake pasipo sapoti kutoka kwa waigizaji wenzake.Huenda walikuwa bize na shughuli zao za kuhakikisha mkono unakwenda kinywani, lakini sidhani kama waigizaji wote, kwa wakati mmoja wanakuwa bize kiasi kwamba wakosekane watu kadhaa wa kumsapoti. Unapata mshangao kidogo unapomuona ni Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ pekee ndiye ambaye amekuwa akienda kila kesi hiyo iliposikilizwa na kumfariji muigizaji mwenzake. Lakini hawa wengine, walionekana kumfariji zaidi kupitia akaunti zao kwenye mitandao ya kijamii, kitu ambacho si sawa.
Matatizo ya kisheria, kama yalivyo yale ya kijamii kama ugonjwa na vifo, ni vitu ambavyo hutokea bila kutazamiwa, kiasi kwamba yeyote yanaweza kumkuta wakati wowote. Inapotokea kwa mwenzio leo, ni dalili kuwa kesho au keshokutwa inaweza kuwa kwako. Kama amabvyo wewe ungefarijika sana kuona wafanyakazi wenzako wakija hospitalini na kukujulia hali pale unapopatwa na matatizo ya kiafya, ndivyo ambavyo hata mwenzako naye anapojisikia pale unapohudhuria udhuru unaomkuta.

Kama kwa mfano siku ya hukumu ile ya kusikitisha ingemkuta akiwa amezungukwa na waigizaji wenzake, bila shaka angejisikia faraja kubwa, kwa kuamini kuwa wenzake wako nyuma yake. Lakini hali hii inaweza kuwa imechangiwa pia na tabia za Lulu mwenyewe kwa namna ambavyo amekuwa akishiriki na wenzake katika matatizo yao, maana wakati mwingine watu hufanya vile ambavyo wao hufanyiwa.

Kama Lulu alikuwa siyo mshiriki katika shida za wenzake, basi hili ni suala la waigizaji wenzake kujifunza, kwani hakuna kitu kinachotia faraja katika matatizo kama unapowaona watu unaoishi nao, unaofanya nao kazi au unaoshiriki nao shughuli yoyote ya kijamii. Na urafiki wa kweli ni pale tunaposhirikiana katika shida, kwa sababu raha huwa zinaandaliwa na kutengenezwa. Shida zinatutaka kujitoa, wakati mwingine kupoteza muda au vitu vyetu kwa ajili ya wenzetu. Sasa unapokuwa mgumu kujitoa kwa wenzako, matokeo yake ndiyo kama haya yaliyomkuta Lulu, kwani licha ya ustaa wake mkubwa, siku ya hukumu yake hakukuwa na muigizaji yeyote mkubwa zaidi ya Dk Cheni aliyekwenda kumfariji.
CREDIT
GPL

Comments

Popular posts from this blog