Alietajwa kufariki ajali ya ndege kumbe yupo hai

Mfanyakazi wa hoteli za kitalii za andBeyond Serengeti, Moses Muhina aliyetajwa kuwa ni miongoni mwa abiria waliofariki dunia katika ajali ya ndege ya Shirika la Coastal Aviation, imebainika alibadili ndege muda mfupi kabla ya safari ili kuwahi kazini.

Muhina ambaye ni mwongozaji watalii katika hoteli hiyo, alikuwa aondoke na ndege ya Coastal Aviation saa nne asubuhi lakini viongozi wa hoteli walimbadilishia ndege, hivyo aliondoka na Air Exel iliyofika salama Serengeti.

Akizungumza na gazeti hili, meneja uendeshaji wa Hoteli ya andBeyond Serengeti Under Canvas, Mussa Matala alisema Muhina ambaye anasomeka kwenye orodha ya ndege kama Maina alikuwa apande ndege hiyo lakini walimbadilishia.

Alisema waliomba aondolewe kwenye orodha ya wasafiri wa ndege hiyo lakini kwa bahati mbaya hadi ndege ilipoondoka jina lake lilikuwapo.

Wakati huohuo, raia watano wa kigeni ambao walifariki dunia katika ajali hiyo, akiwamo rubani Dewald Raubenheimer raia wa Afrika Kusini, ambaye kwenye orodha ya awali ya waliofariki jina lake halikuwapo anatarajiwa kusafirishwa leo.

Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya mkoa ya Mount Meru, Francis Costa alisema miili mitatu kati ya 11 imechukuliwa na ndugu zao.

Alisema miili iliyochukuliwa ni ya ndugu wawili waliokuwa wakurugenzi wa Masai Wondering, Nasibu na Shatri Mfinanga.

Mwingine ni wa Joyce Mkama ambaye alikuwa mfanyakazi wa Hoteli ya Serena.

“Uchunguzi wa miili ya wageni kutoka nje ya nchi unaendelea na ukikamilika itasafirishwa kwa mazishi katika nchi za Afrika Kusini, Ujerumani na Italia,” alisema.

Ndege hiyo namba 5H-EGG aina ya Cessna Grand Caravan ilianguka baada ya kugonga kingo za creta ya Empakai, umbali wa mita 3,250 kutoka usawa wa bahari ikitoka Kilimanjaro kwenda Hifadhi ya Serengeti.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema uchunguzi unaendelea kuhusu ajali hiyo.

Comments

Popular posts from this blog