Wolper Anapozomeana na Kivuli Chake

Jacqueline Wolper Massawe, aliye pia na a.k.a nyingi zikiwemo za Gambe na Amber Rose wa Bongo.

MIONGONI mwa waigizaji wa kike niliowahi kufanya naye kazi kwa kipindi kirefu na kwa ukaribu zaidi ni pamoja na mrembo Jacqueline  Wolper Massawe, aliye pia na a.k.a nyingi zikiwemo za Gambe na Amber Rose wa Bongo. Mkononi nimefumbata miaka saba sawa tangu nianze kazi ya uandishi wa habari, kwenye magazeti haya pendwa.

Ninao uzoefu mkubwa kwa kuwafahamu watu wengi maarufu kwa maana ya maisha yao ndani na nje ya kazi zao, nawajua sana hususan wasanii wa filamu ambao nafanya nao kazi mara kwa mara. Hata wengi wao wananijua vyema , kwenye eneo la kazi kwamba huwa siruki sentensi kwenye kuanika ukweli. Hivi karibuni, Wolper alikaririwa na mmoja wa waandishi wenzangu akisema kitendo cha kumshika na kumbeba mtoto wa mwigizaji mwenzake, Faiza Ally kimemuondolea gundu ya kutopata mtoto hivyo na yeye kutarajia kupata wa kwake mwakani.

Sawa, Wolper yuko sahihi lakini mbona maelezo hayo yanakanganya na kuzua maswali mengi yanayoumiza ubongo? Nitafafanua. Mwishoni mwa mwaka jana (2016), nikiwa nafanya kazi kwenye ofisi zingine (jina nalipaka oili), kama mwanahabari niliwahi kufanya naye mahojiano kwa njia ya simu (kumbukumbu zipo) na miongoni mwa maswali ambayo nilimuuliza ni pamoja na hilo la kutokuwa na mtoto lakini majibu yake yalinipa picha halisi kwamba Wolper hayuko tayari kupata mtoto kwa sasa hata ndani ya miaka mitatu au mitano ijayo kwa kile alichosema umri wake bado sana.
Ngoja nikumbushie kidogo sehemu fupi ya mazungumzo yangu na yeye kwa siku hiyo. Mimi: Hivi kwa nini Wolper unashindwa kuolewa na ukatulia na mume ili maisha yasonge? Wolper: Kwani wewe umeoa?

Mimi: Bado. Wolper: Sasa kama bado kwa nini unaniuliza mimi nisiolewe, inakuwaje babu wewe au unataka kunichuria (neno la kisela lenye kuonesha kuudhika). Mimi: Binafsi umri wangu bado.
Wolper: Kwani wewe unajua umri wangu? Hebu niambie una miaka mingapi?
Mimi: Nina miaka (nikamtajia umri wangu). Wolper: Mimi bado mdogo sana, sijapanga kuolewa kwa sasa, natafuta maisha kwanza aise.
Mimi: Hivi Wolper una mtoto?
Wolper: (kwa sauti ya ukali na ya juu zaidi) Bwana eeeeh hivi (akilitaja jina langu), umetumwa? Nizae kabla ya muda wangu ili iweje? Nitazaa muda ukifika lakini siyo leo wala miaka mitatu ijayo labda mitano, maisha yenyewe magumu namna hii halafu tunaleteana habari za kuzaa hapa, unakuwaje wangu? Au unataka nikujibu vibaya tuanze kuandikana vibaya? Sitaki bwana habari hizo… (anaendelea…) Tafuta maswali mengine ya kuniuliza ndipo unipigie simu sawa?

Ni kweli raha ya kila mwanamke ni kuzaa lakini kila jambo lina wakati na mimi niko fiti nikihitaji kuzaa ni wakati wowote tu, mayai yangu yako active (hayana tatizo lolote), tena nikitaka kuzaa wala sitamuuliza au kumhusisha mwingine ni mimi na Mungu wangu tu. Mimi: Sasa ukiwaona wanawake wenzako wamebeba watoto wao huwa huumii na kujisikia vibaya?
Wolper: Niumie nini sasa? Kawaida na nimeshasema siyo kwamba sina uwezo wa kuzaa la hasha. Naweza na sina mkosi kwa hilo na unielewe maana naona kama unanichanganyia habari tu hapa, hebu niache nifanye shughuli zangu sawa? (anakata simu na kuizima kabisa). Nimelazimika kukumbushia sehemu fupi sana ya mazungumzo yangu na Wolper kwa siku hiyo ili kama atasoma hapa aone ni kwa namna gani niko sawia na ninachokiandika hapa.

Leo Wolper anasema amemshika mtoto wa Faiza (Li) eti ni ishara kwamba ameondoa gundu ya kutopata mtoto! Hiyo gundu imetoka wapi wakati aliwahi kukana kabisa kwamba hana gundu na hajaamua tu kuzaa kwa kuwa umri bado na wingi wa majukumu ambayo yanambana kufanya hivyo, huku akisisitiza ndani ya miaka mitano ijayo? Wolper anataka kumchezea nani akili? Wakati mwingine mimi huwa nalazimika kuandika ukweli juu ya mambo ambayo hata wahusika huwa hawapendi yaanikwe ingawa ni ukweli na ndiyo maana uhusiano wangu na wasanii wengi wasio waelewa siyo mzuri kwa sababu kwenye kazi yangu ya kuandika huwa simhofii wala kumuonea mtu.


Naamini kabisa kwamba kama Wolper angeniona kwenye shughuli hiyo ya mtoto wa Faiza, kama ana kumbukumbu nzuri asingeweza kusema kwamba nimemshika na kumbeba Li hivyo nimetoa gundu, kama angefanya hivyo ningeamini pia kwamba analo tatizo kubwa la KUSAHAU! Nimsihi tu Wolper awe makini na kauli anazotoa wakati wa mahojiano na waandishi wa habari, kwani kujichanganya kwake kwa kauli kunaweza kumshushia heshima yake kwa jamii ambayo inaaminika kwamba yeye ni kioo cha jamii kujitazamia kwa ajili ya kuwa na mienendo mizuri.

Kitendo cha ulimi mmoja kuwa na kauli mbili hutafsiri jambo moja tu. Mtu husika hajiamini na hana msimamo juu ya utendaji wake wa mambo, jambo ambalo kama nilivyosema huko nyuma kwamba, hupunguza mno heshima na wakati mwingine hata thamani ya mtu kwa hadhira. Wolper kama anahisi ana tatizo kwenye suala zima la uzazi, ni bora tu akaweka wazi ili kama kuna uwezekano wowote wa kusaidiwa iwe hivyo au asimamie eneo moja kwamba bado hana mpango wa kuolewa wala kuzaa, lakini kuliko asubuhi aseme sina mpango na sifikirii kabisa kuzaa halafu kabla hata njiwa hajameza punje ya mtama anajitokeza kwa mwanahabari na kusema ametoa gundu kwa kumbeba mtoto.

Kufanya hivyo hakumsaidii kwa lolote na chochote zaidi ya kujichora na kujianika kwa watu, vinginevyo Wolper anajaribu kukizomea kivuli chake, ambapo tafsiri yake ni kwamba anajidanganya yeye mwenyewe kwani kama ana tatizo na bado anataka tuamini kwamba yuko sawa au kinyume chake, huko ndiko kujidanganya na maana yake kwa wale wajuzi wa misemo huhitimisha kwa kuainisha kwamba mtu wa namna hiyo hufananishwa kama anayekizomea kivuli chake. Nawalisilisha.

Comments

Popular posts from this blog