Mtoto wa Mwalimu Mkuu Aanika Alivyomkuta Baba Yake Amejinyonga
MTOTO Frank Benedicto (14) ni mtoto mkubwa wa Mkuu wa Sekondari ya Migukulama, Benedicto Lweikiza (45) aliyejinyonga juzi, amesema alitahamaki kumkuta baba yake akiwa amening’inia darini.
Lweikiza alijinyonga hadi kufariki juzi saa tisa alasiri katika mtaa wa Kilabela Kata ya Nyatukala wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Mwalimu huyo alikuwa anafundisha Sekondari ya Migukulama iliyopo Kata ya Nyanzenda Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.
Mtoto wa marehemu huyo aliyekuwa akiishi na baba yake kwenye nyumba hiyo, anasoma kidato cha kwanza katika Sekondari ya Sima iliyopo wilayani hapo, alisema baada ya kutoka shuleni alikuta mlango wa nyumba yao upo wazi hivyo akadhani baba yake atakuwa kwa majirani.
“Asubuhi niliagana vizuri na baba yangu wakati nikienda shuleni, jioni niliporudi ndipo nikakuta baba amejinyonga juu ya dari na kabla sijagundua kitu chochote nilikuta mlango wa nyumba upo wazi nikadhani yupo kwa majirani nilipoingia chumbani sikuamini nilichokiona mbele yangu,” alisema
Alisema baada ya kuona hivyo alitahamaki na kuanza kupiga kelele ndipo majirani walifika kushuhudia tukio hilo.
Mmoja wa majirani hao, Silvesta Juma alisema kabla marehemu hajajinyonga walikuwa wote asubuhi wakibadilishana mawazo na wakaachana salama hivyo alishtuka kukuta amejinyonga.
Martha Mabula ni mwanafunzi wa kidato cha pili shule aliyokuwa akifundisha mwalimu huyo, alisema “Kifo cha mwalimu wetu kimeshtua wengi na kuacha simanzi kubwa na pengo hili litachukua muda kuliziba.”
Msemanji wa familia hiyo, Martin Kalemera alisema kuwa maiti atasafirishwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Sengerema ilipokuwa imehifadhiwa na kwenda kuzikwa leo kijijini kwao Kasisa Buchosa.
Alisema hadi sasa hakuna taarifa rasmi zilizopatikana za ndugu yao kujinyonga kwa sababu hakuacha ujumbe wowote wala familia haikuwa na taarifa zozote mbaya dhidi ya ndugu yao.
Alisema marehemu ameacha watoto watatu. Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema kuwa vyombo vya Dola vinafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo na kusema kuwa watatoa taarifa baadaye baada ya uchunguzi kukamilika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jeshi la polisi linaendela kufanya uchunguzi wa kifo hicho.
Comments
Post a Comment