MHASIBU UBALOZI WA TANZANIA MSUMBIJI APANDISHWA KORTINI KISUTU
MHASIBU wa Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Joyce Moshi (56) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka tisa ikiwemo ya utakatishaji fedha wa dola za Marekani 150,000.
Moshi ambaye ni Mkazi wa Temeke alifikishwa mahakamani hapo leo na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili wa Serikali, Saimon Wankyo alidai kuwa Oktoba 25, 2016 katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Maputo nchini Msumbiji, alighushi barua ikionesha kwamba Ubalozi wa Tanzania Nchini Msumbiji Umeielekeza Benki ya MIllenium kupeleka Dola za kimarekani elfu kumi katika akaunti inayomilikiwa na Joyce Moshi akijua yakuwa siyo kweli.
Inadaiwa barua hiyo ilionyesha kuwa ubalozi umeelekeza Benki ya ya Millennium BIM ya Maputo, kuhamisha dola za Marekani 10,000 kutoka akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inayomilikiwa na Mushi akaunti zote zipo kwenye benki hiyo iliyopo Julius Nyerere Maputo, wakati akijua si kweli.
Pia inadaiwa Februari 10, 2017 katika ofisi za Ubalozi zilizopo Maputo nchini Msumbiji, alighushi barua nyingine kuonesha kuwa ubalozi umeelekeza Benki ya ya Millennium BIM ya Maputo, kuhamisha dola za Marekani 10,000 kutoka akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inayomilikiwa na Mushi akaunti zote zipo kwenye benki hiyo iliyopo Julius Nyerere Maputo, wakati akijua si kweli.
Wankyo alidai Aprili 12, mwaka huu katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Maputo nchini Msumbiji, Moshi alighushi barua ya Aprili 12, 2017 kuonesha kuwa ubalozi umeelekeza Benki ya ya Millennium BIM ya Maputo, kuhamisha dola za Marekani 40,000 kutoka akaunti namba 79667362 kwenda akaunti namba 182283177 inayomilikiwa na Mushi na kwamba akaunti zote zipo kwenye benki hiyo iliyopo Julius Nyerere Maputo, wakati akijua si kweli.
Katika mashitaka ya nne, inadaiwa Oktoba 25, 2016 katika Benki ya Millennium BIM iliyopo tawi la Julius Nyerere Maputo nchini Msumbiji, Moshi aliwasilisha kwa benki hiyo nyaraka za kughushi ambayo ni barua ya Oktoba 25, 2016 kuonesha kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji umeelekeza benki hiyo kuamisha dola za Marekani 10,000 kutoka kwenye akaunti ya benki hiyo kwenda kwa Mushi.
Wankyo aliendelea kudai kuwa Februari 10, mwaka huu katika benki hiyo, Moshi alitoa nyaraka za uongo kuonesha kwamba Ubalozi umeelekeza kuamisha dola za Marekani 10,000 kwenda kwenye akaunti ya Mushi.
Pia inadaiwa Aprili 12 mwaka huu, maeneo ya benki hiyo aliwasilisha barua ya Aprili 12, mwaka huu kuonesha kuwa ubalozi umeelekeza kuamisha dola za Marekani 40,000 kwenda kwenye akaunti yake.
Katika mashitaka ya saba, Wankyo alidai mshitakiwa huyo katika tarehe tofauti kati ya Oktoba 25, mwaka jana na Aprili 12, mwaka huu akiwa mtumishi wa umma kama Mhasibu wa Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji, aliiba dola za Marekani 150,000 mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa kati ya Oktoba 25, 2016 na Aprili 12, 2017 katika ofisi za ubalozi huo, Moshi alijipatia dola za Marekani 150,000.
Katika mashitaka ya tisa, inadaiwa kati ya Oktoba 25, 2016 na Aprili 12, 2017 katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo Maputo nchini Msumbiji na Benki ya Millenium BIM tawi la Julius Nyerere Maputo, alijipatia dola za Marekani 150,000 wakati akijua fedha hizo ni zao la kughushi.
Comments
Post a Comment