Mambo 10 Utayaona Leo Uwanja wa Uhuru…Simba vs Yanga
YANGA na Simba zinakutana leo Jumamosi kila moja ikiwa imepania kushinda mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Pamoja na yote, watani wanapokutana kunakuwa na burudani nyingi sana ambazo zinatofautisha aliye uwanjani na atakayeangalia katika runinga.
Kwenye Uwanja wa Uhuru, idadi ya mashabiki wanaotakiwa kuingia ni 23,000 tofauti na 60,000 kwenye Uwanja wa Taifa. Pia kumbuka mechi hii ya watani inarejea kwenye uwanja huo baada ya kipindi kirefu.
Kutakuwa na mengi ambayo yatajitokeza ndani na nje ya uwanja, lakini nakupa 10 tu ambayo kwa asilimia 90 utayaona.
Wasio na tiketi:
Watu watajitokeza wengi zaidi kuliko idadi ya wale walio na tiketi na watajazana nje ya uwanja na kusababisha kero kubwa nje ya uwanja.
Bado kuna tabia ya watu kuamini kuwa wanapokwenda uwanjani kuna nafasi ya kuingia angalau kwa njia za mkato. Hivyo hawatakubali kuondoka mapema badala yake wataendelea kujaribu kutafuta njia ya kuingia kadiri itakavyowezekana.
Watu wa dezo:
Kuna mashabiki wa soka ambao wataonekana kwenye Uwanja wa Taifa (labda makala hii iwaponze).
Hao watakuwa wakishuhudia mechi hiyo inayoendelea kwenye Uwanja wa Uhuru bila ya kiingilio kwa kisingizio kuwa ni wafanyakazi wa uwanja huo. Inawezekana wako wataitumia nafasi hiyo kujiingizia kipato.
Hawataona mechi:
Kuna asilimia kubwa ya watakaokwenda uwanjani hawataona mechi hiyo ya watani.
Kwani hawatakuwa na tiketi lakini watakuwa na matumaini ya kujipenyeza ili kuona mechi hiyo. Hii itawafanya wajikute hadi mapumziko hawajaingia na ikiwezekana kipindi cha pili kitawakuta hapo wakishangilia mabao kwa hisia au kuhadithiwa kwa kuwa hawataweza kuingia.
Mzozo jukwaa kuu:
Baada ya zaidi ya miaka 10, mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga imerejea katika Uwanja wa Uhuru. Wako mashabiki hawakuwa wamewahi kuanza kuingia uwanjani timu hizo zikicheza Uwanja wa Uhuru wakati huo Uwanja wa Taifa.
Hao watapata shida kubwa kutokana na aina ya ushangiliaji zinapokutana Yanga na Simba kwenye uwanja huo na hasa jukwaa kuu kwani wanakuwa karibu na mazoezi ya Uwanja wa Taifa yanaweza kuwasumbua na kutakuwa na mizozo mingi sana.
Tafrani ya mgawo:
Kama nilivyoeleza, mechi hiyo imerejea tena Uwanja wa Uhuru na inachezwa kwa mara ya kwanza kukiwa na jukwaa la mzunguko. Kwa wanaokumbuka kabla kulikuwa na jukwaa kuu ambalo lipo hadi sasa, Jukwaa la Kijani maarufu kama Green Stand ambalo lilivunjwa na mzunguko ambalo watu walikuwa wakisimama.
Upande wa Green Stand na mzunguko ndipo palipojengwa jukwaa jipya. Hivyo Simba na Yanga hazijawahi kukutana kukiwa na jukwaa hilo. Hivyo lazima kutakuwa na shida ya kugawana wapi sahihi pa kukaa na hawa wanaishia wapi na lazima askari polisi watalazimika kuingilia kati.
Ajibu ugumu:
Tukirejea uwanjani, mshambuliaji Ibrahim Ajibu wa Yanga atakuwa na wakati mgumu kwa kuwa mashabiki wa Simba watafurahi sana kumuona akiharibu na ikiwezekana kumzomea kila mara na atalazimika kufunga au kutoa pasi ya bao ili kuwanyamazisha.
Hali kadhalika, Emmanuel Okwi naye atakumbana na hali hiyo kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao wasingependa kumuona hata akicheza mechi hiyo.
Makocha:
Makocha wote wawili, Joseph Omog wa Simba na George Lwandamina wa Yanga watakuwa katika wakati mgumu sana na utaona wakiwa na presha muda mwingi hawatatulia katika mabenchi yao.
Kila mmoja anajua kupoteza mchezo wa leo kunaweza kukawa ni njia ya kutokea. Hivyo lazima atakuwa akisimama kila mara kuhakikisha anaweka mambo sawa na kama atazidiwa na kuona anashindwa kufanya hivyo, mara nyingi watawatuma wasaidizi wao ikiwezekana wasikae karibu muda wote wa mechi.
Mfungaji:
Timu yoyote inaweza kushinda kwa kuwa timu hizo zinafanana sana hasa kitakwimu kulingana na mechi zilizocheza.
Uwezekano mkubwa wa wafungaji kutokuwa Okwi wala Ajibu kwa kuwa kila timu itafanya kazi kubwa ya kuwalinda halafu ikajisahau na kutoa nafasi kwa wengine.
Kadi:
Mechi ya leo ina nafasi kubwa ya kadi hasa kama timu itashindwa kufunga au kutimiza inachotaka.
Inawezekana kabisa wachezaji wa Simba wakaanza ‘kupanik’ kama watakufungwa mapema au Yanga wakawa hivyo kama watafungwa halafu wakashindwa kusawazisha katika kipindi wanachotarajia.
Hali hii inaweza kumsababisha mwamuzi kutoa kadi za njano au hata nyekundu kutokana na hali ya kupanik kutokana na presha ambayo wachezaji wanaipata.
Ushirikina:
Hili halina nafasi kubwa lakini kwa mfumo wa uwanja ulivyo tofauti na Uwanja wa Taifa, kuna nafasi kubwa ya mambo ya kishirikina kujitokeza.
Uwanja wa Uhuru uko wazi zaidi na haufichi mambo ambayo yamekuwa yakifanyika hasa kuhusiana na imani chafu za kishirikina. Inawezekana timu hata zikawa tayari kutozwa faini ili kufanya mambo hayo “kujiridhisha”.
Comments
Post a Comment