Majambazi Walivyomtwangwa Risasi Mwenzao Mbele ya Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah.
ROBERT Massawe (51), mkazi wa jijini Dar es Salaam, ambaye polisi wanadai ni mtuhumiwa wa uporaji na mauaji, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni wahalifu wenzake.
Kabla ya kuuawa katika majibizano ya risasi, mtuhumiwa huyo anadaiwa alikamatwa akiwa na SMG yenye risasi 24, simu 19 zilizoporwa maeneo mbalimbali na laini za simu 58.
Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah imesema mtuhumiwa aliuawa na wenzake saa tisa usiku wa kuamkia jana wilayani Rombo.
Alisema mtuhumiwa pamoja na mkewe walikamatwa jijini Dar es Salaam na baada ya kuhojiwa na polisi inadaiwa alieleza matukio ya ujambazi aliyoshiriki na alikubali kuwaonyesha mahali alipoficha bunduki.
Polisi imesema simu tatu kati ya 19 wamegundua ziliporwa Moshi na moja alikuwa akiitumia mkewe ambaye anashikiliwa Dar es Salaam.
Kamanda Issah alisema aliwaeleza polisi kuhusu mpango wa kufanya tukio la ujambazi katika Kijiji cha Chilio, Kata ya Holili wilayani Rombo jana alfajiri.
Alisema askari walifuatana naye chini ya ulinzi hadi Moshi kwenye dampo lililopo jirani na kiwanda cha ngozi ambako bunduki ilifukiwa ardhini ikiwa na risasi 24.
“Chini ya ulinzi wa askari kanzu, alipowaona wenzake alipiga kelele kuwajulisha polisi walikuwepo eneo hilo,” alisema.
Kamanda Issah alisema kelele ziliwafanya watuhumiwa hao kukimbia huku wakifyatua risasi hovyo na baadhi zilimpiga Massawe mkono wa kushoto, mgongoni na mguuni hivyo kusababisha kifo chake.
Polisi imesema mtuhumiwa alishiriki matukio manane ya uporaji wa fedha na mauaji kwa kutumia silaha na amewahi kufungwa kwa ujambazi lakini aliachiwa baada ya kukata rufaa.
SOURCE:GPL

Comments

Popular posts from this blog