KAULI YA LOWASSA BAADA YA LAZARO NYALANDU KUIHAMA CCM

ALIYEKUWA Mgombea Urais wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amemkaribisha aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, ambaye amejivua uanachama na kuachia nyadhifa zote alizokuwa nazo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akionyesha kuwa na furaha alipozungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Lowassa hakuwa na maneno mengi, akiyafupisha kwa kusema “tumelamba dume”.
Nyalandu (47), ambaye pia alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alitumia nafasi hiyo kuomba kujiunga na Chadema, akisema anaiomba imfungulie mlango.
Dakika chache tangu Nyalandu aombe kujiunga na Chadema, Lowassa alimkaribisha waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii huku akisema mwanasiasa huyo amechelewa kujiunga na upinzani.
“Mbona amechelewa? Alitakiwa awe amejiunga muda mrefu, tena hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu. Ninamkaribisha sana kwa sababu ni mwanasiasa mzuri na anayejua majukumu yake,” alisema Lowassa ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza katika Serikali ya Awamu ya Nne.
“Nyalandu ni hazina, ni mbunge imara na ni mwanasiasa wa mfano,” alisema Lowassa, ambaye alijiunga na Chadema mwaka 2015 na kuwania urais kupitia muungano wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa).
Lowassa alimsifu Nyalandu kwa kuisaidia jamii na akatoa mfano jinsi alivyosaidia watoto watatu wa Shule ya Lucky Vincent waliokwenda kutibiwa Marekani baada ya kupata ajali ya basi iliyoua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja.
“Nyalandu ana contacts (anafaham watu wengi) nyingi na jumuiya ya kimataifa, ni bidhaa nzuri kuwanayo,” alisema Lowassa, ambaye katika uchaguzi wa urais alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072,848 (asilimia 39.97) ikiwa ni rekodi ya kura nyingi kwa upinzani tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe mwaka 1992.

Comments

Popular posts from this blog