Jaji Warioba ashauri Viongozi wakutane na Wazungumze
Waziri Mkuu wa zamani, Joseph Warioba amewataka viongozi wa kisiasa
kujenga utamaduni wa kukutana wanapogundua kuna matukio yanayoashiria
uvunjifu wa amani.
Jaji Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
amesema waasisi wa Taifa walijenga umoja na misingi ya maendeleo ambayo
kuna dalili ya kutoweka.
Amesema hayo leo Alhamisi Oktoba 26,2017 jijini Dar es Salaam akifungua
mdahalo wa mashauriano juu ya kuhamasisha, kusisitiza, kulinda na
kudumisha amani, umoja na maridhiano nchini.
Amesema viongozi wa dini wamekuwa na kawaida ya kukutana wanapoona mambo
hayaendi sawa jambo ambalo ni zuri na linapaswa kuendelea.
Jaji Warioba amesema kuna viashiria vya kutoweka kwa amani na viongozi
wa kiserikali na kisiasa wanapaswa kuiga kile wanachofanya wenzao wa
dini.
"Amani ikitoweka kuirudisha ni shida au kuiendeleza. Viongozi hasa hawa
wa kisiasa wawe wepesi kukutana na kuzungumza, tuache malumbano na hasa
viongozi wa kisiasa na tukiendelea wanaweza kutufikisha pabaya," amesema
Jaji Warioba.
Amesema ,"Hata kama wanatumia mitandao ya kijamii au vyombo vya habari
kujibizana ni muhimu viongozi wa kisiasa wawe tayari kukutana kama
wanavyofanya viongozi wa dini."
Jaji Warioba amesema, ''Nchi haiwezi kuendeleshwa kwa huyu kuongea hiki,
huyu naye anamjibu kupitia vyombo vya habari. Hapana, hawa watu wakae
wazungumze."
Amesema Watanzania wanapaswa wakae pamoja, waone matatizo na
kuyazungumza na wafikie muafaka kwa kuwa hakuna njia nyingine ni kukaa
na kuzungumza.
"Tunayo matatizo katika nchi yetu, hawa viongozi wa kisiasa lazima
wakutane wazungumze na kikao hiki tujadili hapa na tupeleke ujumbe wetu
kwa wote wanaohusika kwa lengo la kudumisha amani yetu," amesema.
Awali, akisoma hotuba ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF),
Joseph Butiku aliye nje ya nchi, Miraji Magai amesema lengo la kikao ni
kutafakari kwa makini unyenyekevu, uhuru na uwazi wa kiwango cha
kutosha, nyufa ndogo au viashiria vinavyoweza kulegeza au kuashiria
kuvunja amani na umoja wa Taifa.
"Vipo viashiria vinavyoweza kutuvunjia umoja na amani yetu. Tutumie
kikao hiki kuvitambua na kukubali kwamba vipo, hivyo tukitafakari kwa
makini vyanzo au asili ya viashiria hivyo," amesema.
Mbali ya Magai, Msaidizi Maalumu wa Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Gallus
Abeid amesema kabla ya kuandaa mdahalo huo walikwenda katika mikoa na
kuzungumza na makundi na viongozi wa kiserikali kuhusu matatizo
yaliyotokea na jinsi ya kuyapatia ufumbuzi.
Chanzo: Mwananchi
Comments
Post a Comment