Hali Ilivyo Jijini Nairobi… Raila Odinga Vs Jeshi la Polisi

POLISI Kikosi cha Kuzuia Ghasia wamefunga eneo lote la viwanja vya Uhuru Park jijini kabla ya mkutano ulioandaliwa na muungano wa National Super Alliance (NASA) kwa ajili ya kiongozi wake mkuu Raila Odinga kutoa tamko zito kuhusu mchaguzi wa marudio kesho.
Maofisa wa polisi wakiwa katika sare zao wamesambazwa muda mfupi baada ya uongozi wa Kaunti ya Jiji la Nairobi kumwandikia kamanda wa Japhet Koome akipinga uwanja huo kutumiwa na Nasa.
Gavana wa Nairobi Mike Sonko amemtaka kamanda Koome kuhakikisha eneo hilo linakuwa na usalama akihofia unaweza kutumika kwa “mkutano ambao haujaruhusiwa”.
“Nimefahamishwa kwamba viongozi wa National Super Alliance (Nasa) wanapanga kutumia viwanja vya Uhuru Park kwa mkutano wa kisiasa leo. Hata hivyo, rekodi za uongozi wa jiji zinaonyesha hawajafuata utaratibu wa kupata kibali kwa ajili ya mkutano huo,” ilisema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Kamanda Koome.
Sonko amesema hakuna mkutano utakaoruhusiwa kwenye viwanja hivyo bila ya ridhaa ya mamlaka husika na kutoka serikalini.
Gavana huyo ameongeza kwamba polisi wahakikishe wanaweka ulinzi ili kuzuia upinzani. “Kwa mamlaka niliyonayo, tafadhari hakikisha mkutano batili haufanyiki bila ya ridhaa yetu na sheria,” amesema.
Mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa Bondo, Odinga aliwataka wafuasi wake kusubiri tamko kabambe Jumatano. Msemaji wake Dennis Onyango amesema asubuhi leo kwamba Odinga ambaye amejiondoa kwenye uchaguzi huo atatoa tamko hilo saa 8:00 mchana.
“Nasa inawaalika wafuasi wote kufika kwa wingi kwa ajili ya tamko zito,” alisema.
Credit: Mwananchi.

Comments

Popular posts from this blog