RAIS MAGUFULI ALIAGIZA JESHI LA WANANCHI KUJENGA UKUTA ENEO LA TANZANITE



              Rais John Magufuli. RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameliagiza Jeshi la Wananchi (JWTZ)kushirikiana na Suma JKT kujenga ukuta eneo lenye madini ya Tanzanite wilayani Simanjiro mkoani Manyara. Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumatano, Septemba 20, 2017 akiwa ziarani mkoani Manyara alipowahutubia wananchi wa Simanjiro akizindua Barabara ya Lami kutoka Kia hadi Mererani.

Nchi hii ni tajiri, tulipewa madini na Mungu ambayo hayapatikani nchi yoyote, lakini hayatusaidii sisi na tunapata shida. Kwa nini tupewe Tanzanite, tena Simanjiro pekee halafu wanachi wapate shida za maji na barabara? Kwa nini tuibiwe? Kwani Mungu alifanya makosa kutupa hayo madini? Haiwezekani, tuanze kubadilika sasa. “Tatizo letu sio vyama, bali ni vipi tunatumia rasilimali zetu.

Tanzanite ingekuwa nchi nyingine, hapa pangekuwa kama Ulaya. Ipo siku Tanzanite haitakuwepo, tutaachiwa mashimo tu! Hakuna haja ya kumung’unya maneno, Tanzanite inaibwa, limekuwa shamba la bibi, tena la mabibi waliokufa miaka ya nyuma. “Naagiza kuwa eneo la madini ya Tanzanite, Mererani ambalo ni Block A hadi Block D liwekwe ukuta, kuwe na mlango mmoja tu.

Juu ya uzio huo kufungwe kamera, hata mtu akimeza Tanzanite itaonekana, ikifichwa kwenye viatu itaonekana, nataka kila mtu apate haki yake,” alisema Magufuli na kuongeza; “Soko la Tanzanite litahamia hapa Simanjiro kutoka Arusha. Kwa kuwa barabara ni ya lami, anayetaka kununua aje aifuate huku, wachimbaji wadogo ruksa kuchimba na mkishachimba Tanzanite mkiwa ndani ya uzio mtauza kwenye maduka humohumo ndani.”

Aidha Rais Magufuli ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuhakikisha inahusika kwenye ununuzi wa madini hayo yanayopatikana Tanzania pekee huku akiwataka wanunuzi kutoka sehemu yoyote duniani wanaohitaji madini hayo, kuyafuata Mererani ili kukuza uchumi wa nchi.

Comments

Popular posts from this blog