“Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejaribu kuvuruga amani yetu”: Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ipo salama na imara na kwamba mtu yeyote atakayejaribu kutaka kuvuruga amani atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Septemba 13, 2017) alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Bw. Mousa Farhang jijini Dar es Salaam.

“Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote kutoka popote atakayejaribu kuvuruga amani yetu. Nawaomba wananchi muwe makini na muendelee kuidumisha amani yetu.”

Amesema kwa sasa Serikali ipo katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi, rushwa, biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na wahujumu uchumi.

Waziri Mkuu amesema licha ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, wameendelea kuwahamasisha wananchi wake kudumisha mshikamano.

Amesema mbali ya kuimarisha amani nchini, pia Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija.

Hivyo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo  vya kuchakata mazao ya  kilimo.

Pia amewakaribisha raia wa Iran kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kama mlima wa Kilimanjaro, fukwe, mali kale na mbuga za wanyama.

Kwa upande wake, Balozi Farhang  ameipongeza Serikali kwa kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi.

Balozi huyo amesema Serikali ya Irani ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi pamoja na vitendo vingine vya kihalifu.

Balozi Farhang ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali ya Tanzania ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu amekubali.

Pia Bw. Farhang amesema aliwahi kutembelea mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro na kusema kwamba ni maeneo mazuri ambayo hajawahi kuyaona tangu azaliwe.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Comments

Popular posts from this blog