Breaking News: Mtekaji Wa Watoto Arusha Auawa Kwa Kupigwa Risasi
Kijana aliyehusika na matukio ya utekaji watoto mkoani Arusha, Samson Petro (18) amefariki dunia kwa kupigwa risasi na polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amethibitisha kutokea kwa kifo hicho alipozungumza na waandishi wa habari.
Kamanda Mkumbo amesema kijana huyo ambaye alikamatwa mkoani Geita alikokuwa amekimbia kabla ya kurejeshwa Arusha alitaka kukimbia alipokuwa anakwenda kuwaonyesha polisi watuhumiwa wenzake wa utekaji saa tano usiku wa jana Jumatano.
Hivi karibuni alipokamatwa mkoani Geita, kijana huyo ambaye sasa ni marehemu alikiri kuwateka watoto wanne mkoani Arusha baada ya kukamatwa mjini Katoro wilayani Geita alikotekeleza tukio lingine la utekaji.
Akizungumza akiwa chini ya ulinzi wa polisi wiki iliyopita, kijana huyo alisema watoto wawili aliwarudisha kwa wazazi wao baada ya kupewa Sh300,000.
Alisema wengine wawili aliwatelekeza mtaani baada ya wazazi wao kutotoa kiasi cha fedha walichotakiwa kutoa.
Kijana huyo alisema alijiingiza katika utekaji watoto kutokana na mahitaji ya fedha. Alisema aliacha shule akiwa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lutozo iliyopo Katoro.
“Naishi na wazazi wangu lakini nao ni masikini, nilifanyahivi ili nipate fedha na nilikua nikimchukua mtoto naandika ujumbe kwenye karatasi, naandika na namba ya simu napeleka karibu na familia ili wanitafute,”alisema.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema walimkamata katika nyumba ya kulala wageni ya Shitungulu iliyopo mjini Katoro.
Mwabulambo alisema polisi mkoani Geita kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha walifanya uchunguzi na kubaini mtuhumiwa alikuwa Katoro.
Alisema walipata taarifa za kutekwa Justin Ombeni (2) Septemba Mosi nyumbani kwao Shilabela ambako mtuhumiwa alienda na kuwakuta watoto wanne wakicheza nyuma ya nyumba. Alisema aliwagawia pipi na kuondoka na Justin.
“Baba wa mtoto alifika kituo cha polisi kutoa taarifa ya mtoto wake kutoweka, tuliwasiliana na polisi Arusha na makao makuu ambako timu ya watu wanne walitoka Arusha na kuungana na yetu ambayo imesaidia kumkamata mtuhumiwa,”alisema Kamanda.
Mwabulambo alisema polisi ilipata taarifa kuwa kijana huyo yupo chumba namba 103 katika nyumba hiyo ya wageni ambako waliweka ulinzi kuizunguka.
Alisema walipoingia chumba hicho walimkuta akiwa na mtoto huyo. Kamanda alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Ombeni Mshana, ambaye ni baba wa Justin alisema mtekaji huyo alimpatia ujumbe mtoto wa jirani uliomtaka kutuma Sh4 milioni na walipokuwa wakiwasiliana na mtuhumiwa alishusha kiwango hadi Sh1 milioni. Alisema polisi walimtahadharisha kwamba asitume fedha hizo.
Kamanda Mwabulambo alisema tukio la kutekwa Justin ni la pili katika kipindi cha miezi minne baada ya mwingine kutekwa. Kesi kuhusu tukio hilo inaendelea mahakamani baada ya mtoto kupatikana.
Watoto ambao Petro anadaiwa kuwaua kwa kuwatumbukiza kwenye shimo la choo ambacho hakijanza kutumika ni Moureen David(6) anayesoma darasa la kwanza shule ya msingi Lucky Vincent na Ikram Salim(3).
Moureen alitekwa Agosti 21 saa 11:00 jioni akiwa anacheza nyumbani kwao eneo la Olasiti, wakati Ikram alitekwa Agosti 26 saa 12:00 jioni akiwa anacheza na watoto wenzake nyumbani kwao Burka, Olasiti.
CHANZO: MWANANCHI
Comments
Post a Comment