WAZIRI MWAKYEMBE AWAPA ‘DAWA’ WASANII BONGO


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na wasanii.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka Wasanii wa Muziki wa Kizazi kipya nchini kuanzisha mfuko wa wasanii kwa lengo la kutatua changamoto ya udhamini inayowakabili.
Ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na Wasanii hao ambacho kilijadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna ya kukabiliana nazo hivyo kuwataka kutokata tamaa
Amesema kuwa kutokana na malalamiko na changamoto mbalimbali zinazowakabili Wasanii, ambazo nyingi zinasababishwa na mikataba inayowanyonya Wasanii katika kazi zao, ni vema sasa Wasanii hao kupitia Chama chao cha Tanzania Urban Music Association (TUMA) kuanzisha mfuko ambao utakua unatoa mikopo kwa Wasanii ili kuwezesha utendaji wa kazi zao pasipo kutegemea wadhamini.

Dkt. Mwakyembe akisalimiana na wasanii.
“Ninafikiri dawa tunayohitaji ni kuanzishe mfuko wa Wasanii ambapo kila Msanii atatakiwa kuchangia fedha. Jambo ambalo litawavutia wadau wengine kuchangia mfuko huo na kuwaondoa katika dhana ya utumwa, na mfuko huo utamsaidia msanii aliyejisajili kupata mkopo bila kutozwa riba yoyote,” alielezea Waziri Mwakyembe.
Aidha, Mwakyembe amesema kuwa Tasnia ya Sanaa ina mchango mkubwa katika kuongeza pato taifa hivyo ametaka tasnia hiyo kurasimishwa ili kupunguza tatizo la ajira na pia kutumika kama chombo maalumu cha kuielimisha jamii kwani kupitia Sanaa wananchi hupata ujumbe kwa urahisi.
Hata hivyo, Mwakyembe ameunda Kamati ya kushughulikia masuala yanayowakabili Wasanii ikiwemo sera na sheria ili kuboresha maslahi ya Msanii. Wasanii wanaounda Kamati hiyo ni Azma Mponda, Niki wa Pili pamoja na Witness Mwaijanga.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Onesmo Kayanda amesema kuwa, ili kuboresha na kukuza tasnia ya muziki nchini ni lazima kuwepo na soko la uhakika la kazi hizo pamoja na tuzo mbalimbali ambazo zitatumika kutia hamasa kwa wasanii.

Comments

Popular posts from this blog