WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA:SERIKALI KULIPA MADENI YA WATUMISHI
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali italipa madeni yote ya Watumishi ambayo yamehakikiwa na kukutwa kuwa ni halali.
Waziri
Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kwenye mkutano uliyofanyika kata ya
Goweko, wilayani Uyui mkoani Tabora na Rais Pombe Magufuli alisitisha
malipo kwa sababu ya zoezi la kubaini watumishi hewa, sasa kazi hiyo
imeshakamilika na yale yaliyobainika kuwa halali yatalipwa huku
akiwataka Watumishi hao wafanye kazi ya kuwadumia wananchi kwa bidii.
"Hivi
sasa tunadhibiti uzalishaji wa madeni mapya ya watumishi, hakuna madeni
ya matibabu, ya likizo au ya masomo. Kila mtumishi anaruhusiwa
kujiendeleza, lakini ni lazima kwanza aandike barua kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri kuelezea nia yake na akikubaliwa, ndipo aanze kutuma maombi
kwenye vyuo. Mtumishi akiamua kuomba chuoni moja kwa moja ndipo alete
madai yale, hatapewa chochote kwa sababu ni nje ya utaratibu," alisema Majaliwa.
Pamoja
na hayo, Waziri Majaliwa amesema serikali imeondoa utaratibu wa
Mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja au cheo
ndipo aanze kupata stahiki zake mpya.
"Hii
imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili
imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa
za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti
kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine
alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo. Mimi nimekuwa kwenye utumishi
wa umma kwa muda mrefu, sijawahi kuona mtu anaandikiwa barua ya
kupandishwa daraja halafu anakataa. Kikubwa ni kwa maafisa utumishi
kuona kama kuna Watumishi wanastahili kupandishwa madaraja, watume
taarifa zao mapema kabla ya tarehe 10 ya kila mwezi ili waingizwe kwenye
mfumo huo. kisha wawaandikie barua za kuwajulisha wahusika. Hata barua
ikichelewa kumfikia mtumishi, mshahara wake hautachelewa na kwa njia hii
tutaepuka kuweka madeni yasiyo na tija", alisema Waziri Majaliwa.
Kwa
upande mwingine, Majaliwa amewataka Watumishi hao kuwahudumia
watanzania bila kujali hali zao kwa kuwa serikali haitamvumilia mtu
mdanganyifu, mzembe, asiye muadilifu na mla rushwa na endapo atabainika
hatoweza kuundiwa tume kwa madai tume zao zinamaliza fedha, bali wakiwa
na ushahidi wa kutosha watamalizana naye hapo hapo.
Comments
Post a Comment