RAS-Dodoma- Wakumbukeni Idara za Elimu katika PlanRep Mpya.


 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dododma  Rehema Madenge akifungua mafunzo ya siku nane kwa wataalamu wa Afya, Mipango na Fedha kutoka Mikoa Mitano chini ya ufadhili wa mradi wa Uimarishaji Mifumo (PS3)
Serikali mkoani hapa imesema ili mpango wa PlanRep uweze kufanikiwa kwa ufasaha hakuna budi kuzijumuisha idara za Elimu katika mafunzo yanayoendelea mkoani Dodoma yanayo wajumuisha wataalam wa mipango pamoja na afya kutoka mikoa mitano ya Tanga, Tabora, Manyara, Singida na wenyeji Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya bajeti kwakutumia mfumo mpya wa PlanRep na FFARS.
Akifungua mafunzo ya siku nane mkoani hapa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bibi Rehema Madenge, amesema moja ya vitu vilivyokuwa vikikwamisha masuala ya bajeti ni pamoja na kutokuwa na takwimu sahihi huku akinyooshea kidole takwimu za idara za elimu.
“Ninatamani sana takwimu za elimu ziwe sahihi hasa katika uwasilishaji wa taarifa za mitihani ili ziweze kuendana na idadi ya wanafunzi na fedha zinazo ombwa, kuepusha madudu yanayo wasilishwa” alisema madange na kuongeza kuwa katika sekta ya elimu ndipo kuna sarakasi ambazo hata mruka sarakasi mwenyewe hata yeye hamjui.
Mkurugenzi wa Mifumo ya Tehama kwenye mradi wa PS3 Desderia Wengaa akitoa maelezo ya Utangulizi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Planrep na FFARS.

Madenge ambaye kwa taaluma ni Mchumi na aliyeshughulika na kuratibu shughuli za bajeti kwa muda mrefu, amesema ili mipango iweze kuendana na mahitaji suala la kuwa na takwimu sahihi haliepukiki na kuamini kuwa chini ya PlanRep mpya itakuwa mwarobaini katika kutatua changamoto hizo.
Madenge amesema mfumo wa PlanRep ulioboreshwa pia unaenda kutumika kuanzia ngazi ya msingi yaani vituo vyetu vya kutolea huduma ambapo utawezesha kuandaa mipango na bajeti kutokana na vipaumbele na mahitaji ya wananchi ambao ndio waathirika.
 
Erick Kitali Mkurugenzi wa TEHAMA, OR-TAMISEMI akielezea kwa ufupi mifumo iliyoboreshwa  ya Planrep na FFARS wakati wa mafunzo yanaendelea Mkoani Dodoma

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa mifumo ya TEHAMA wa PS3, Desderi Wangaa, amesema, PlanRep mpya iliyoboreshwa imefanyia kazi changamoto kwa kuhakikisha kwamba mipango na bajeti unaingizwa kwa kila mtoa huduma, na unaingiza namba za utambulisho kwa kila mtoa huduma mmoja mmoja kwa kila sekta lakini pia mfumo huu umeweka nafasi ya kila mtoa huduma kuainisha matokeo yanayotegemewa (Service Outputs).
Pichani ni Mgeni Rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Rehema Madenge (Katikati mbele) akiwa na wakufunzi wa mafunzo hayo.(Picha zote na Ofisi ya Rais TAMISEMI)
Awali akitoa maelezo ya utangulizi, Mkurugenzi wa TEHAMA wa OR-TAMISEMI, Erick Kitali, alisema mfumo umezingatia mahitaji ya idara zote za mamlaka za serikali za mitaa na ambao ni fungamanifu unaotumia muda mfupi kukamilisha kazi za uratibu wa bajeti na taarifa za hesabu toka vituo vya huduma.

Comments

Popular posts from this blog