Rais Uhuru Kenyatta Aruhusu Maandamano ya Wanaopinga Ushindi Wake
Rais Uhuru Kenyatta
huenda akaingia katika vitabu vya kumbukumbu na historia kwa marais wa
Afrika kwa kuamua kuruhusu maandamano ya amani kupinga ushindi wake
alioupata katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.
Kenyatta amewataka polisi kujizuia
kutumia nguvu kubwa na badala yake wawape ulinzi wakati wa maandamano
hayo ya amani na yanayoruhusiwa kisheria kwa watu ambao hawafurahii
matokeo ya uchaguzi uliopita.
Rais Kenyatta alisema hayo jana alipokuwa akitoa ujumbe kwa wagombea walioshindwa katika uchaguzi huo uliofanyika Jumanne iliyopita.
Kenyatta alisema hayo akiwa Jengo la Harambee alikokwenda kukutana na Kamati ya Maandalizi ya Hafla ya kuapishwa kwake.
Katika ujumbe huo uliomlenga zaidi
Raila Odinga aliyekuwa mgombea urais kupitia muungano wa Nasa, Kenyatta
aliwataka wagombea wote ambao hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi
wachukue hatua zilizobainishwa na Katiba ili kupata wanachotaka.
“Marafiki zetu ambao hawataki
kukubaliana na matokeo … tumenyosha mkono wetu wa udugu kwao … watumie
njia zozote zilizobainishwa katika katiba kuelezea kutoridhishwa kwao,” alisema.
“Wale wanaotaka kushawishi wengi
wagome wanaweza kufanya hivyo, lakini kwa kuzingatia vifungu vya sheria.
Mwishoni mwa siku sisi sote ni Wakenya. Hakuna haja ya kudhuriana.
Hakuna haja ya kuharibiana mali…tunawashukuru polisi kwa kazi nzuri
lakini waendelee kujizuia.”
“Polisi wako tayari kuwalinda
wakati mnafanya maandamano na wale waliochukia waelewe kwamba hawahitaji
kibali changu wala cha Jubilee kufanya maandamano ya amani.”
Hata hivyo, alitoa onyo kali kwamba
serikali haitavumilia maandamano yatakayosababisha vifo na uharibifu wa
mali za watu kutokana na vurugu.
Vilevile alitoa onyo dhidi ya
waporaji na waharibifu wa mali katika baadhi ya maeneo ya nchi, ambako
yameripotiwa maandamano baada ya uchaguzi.
“Wakenya wengi wamesema uchaguzi
umepita na wamerejea kazini. Hawataki maandamano ya ghasia. Msivuruge
maisha ya watu wengine. Kama serikali hatutaruhusu uharibifu wa mali
wala upotevu wa maisha na uporaji.”
Rais Uhuru alitoa kauli hiyo baada ya
viongozi wa muungano wa Nasa kuhamasisha wafuasi wao kukataa matokeo
yaliyompa ushindi Uhuru na makamu wake, William Ruto.
Baada ya kazi ya kuhesabu kura
kukamilika, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilimtangaza Kenyatta
kuwa mshindi kwa kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27.
IEBC ilisema mgombea urais kwa
muungano wa Nasa, Raila Odinga alipata kura 6,762,224 sawa na asilimia
44.74 matokeo ambayo wanayapinga.
Wakiitikia wito wa viongozi wao kati
ya Jumatano na Jumamosi maeneo, ambayo ni ngome ya upinzani ya Kisumu,
Kibera, Homabay na Migori yalikumbwa na vurugu na soko la Garissa
lilichomwa moto.
Nasa walidai kwamba, kwa mujibu wa
vyanzo vyao kutoka ndani ya IEBC Raila alishinda kwa kura milioni nane
akifuatiwa na Uhuru. Walidai wizi huo ulifanikishwa kwa kudukua kompyuta
iliyokuwa inahifadhi matokeo na kumbukumbu nyingine.
Juzi, akizungumza na wafuasi wake
waliojitokeza kwa wingi katika eneo la Kibera, Raila aliwataka wafuasi
wake wote kususia kazi jana ili kuomboleza vifo vya waliouawa katika
makabiliano na polisi.Pia, alisema atatoa msimamo leo wa nini cha
kufanya.
Katika kile kinachoonekana kuwa ni
kutii wito wa serikali, watu walionekana kupuuza wito wa Raila wa
kususia kazi kuomboleza watu waliouawa katika makabiliano kati ya polisi
na waandamanaji waliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi wa urais.
Wengi walionekana barabarani wakirejea kwenye shughuli zao jana na kuendelea na maisha ya kawaida.
Comments
Post a Comment