Rais Museveni Abadilisha Tarehe Yake wa Kuzaliwa
Kwa muda mrefu sana kumekuwa na mijadala hasa katika mitandao ya
kijamii nchini Uganda kuhusu umri halisi wa Rais wa nchi hiyo, Yoweri
Kaguta Museveni.
Kwa mara kadhaa serikali ya Uganda imekuwa ikinukuliwa ikisema
kwamba Rais Museveni alizaliwa mwaka 1944, lakini kabla ya uchaguzi mkuu
wa mwaka jana vyama vya upinzani vilikuwa vikimkosoa Rais Museveni
kwamba anadanganya kwa kusema ana miaka 71. Vyama hivyo vilidaiwa kuwa
alikuwa na zaidi ya umri wa miaka 75 na asingeweza kugombea tena.
Lakini mjadala mpya umeibuka ambapo Ikulu ya Uganda imechapisha
nyaraka kwenye ukurasa wake wa Facebook zinazoonyesha kwamba nyaraka za
ubatizo wa Rais zimeandikwa tarehe yake ya kuzaliwa ambayo ni 3 Agosti
1947 na hivyo sasa ana miaka 70.
Kwa minajili hiyo, Rais Museveni atakuwa na umri wa maika 74 wakati
Uganda itakapofanya uchaguzi mwingine mwaka 2021 na hivyo ataweza
kugombea tena katika awamu ya sita.
Museveni alibadilisha katiba ya Uganda mwaka 2006 ili kuweza
kugombea awamu ya tatu. Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la nchini
humo, Rais amewahi kusema kwamba hafahamu tarehe yake ya kuzaliwa.
“Wazazi wangu hawakwenda shule na hivyo hawakujua tarehe,” alinukuliwa Rais Museveni mwaka 1997 alipokuwa akitoa taarifa zake katika mahojiano maalum.
Mkanganyiko huu umekuja ikiwa ni
takribani wiki moja tangu Rais Museveni aliposema kuwa katika kipindi
cha miaka 31 alichokuwa madarakani hajawahi kuugua.
“Umewahi kusikia Museveni ameumwa na
miguu yake kuning’inizwa hospitalini kwa miaka 31 iliyopita? Hii ni kwa
sababu nafuata hatua za msingi za afya ambazo zimenisaidia kuepukana na
magonjwa. Magonjwa haya yanaweza kuzuilika,” alisema Museveni akitamba kwamba afya yake ni imara.
Comments
Post a Comment