Paparazzi Maarufu Akutwa Amejinyonga
Wakazi wa Chalinze na vitongoji vyake mkoani hapa, Jumatano iliyopita walikumbwa na simanzi baada ya paparazzi na mpiga picha wao maarufu, Mogela Msimbe kukutwa amejinyonga kwenye nyumba iliyokuwa ikiendelea kujengwa muda mfupi baada kuaga kuwa anakwenda kushuhudia tukio la wapenzi wawili waliodaiwa kunasiana wakizini ambalo nalo lilidaiwa kutokea siku hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyekataa kutaja jina lake, alisema siku ya tukio marehemu ambaye alikuwa mpiga picha na mwandishi wa habari wa kujitegemea alionekana kuwa na mawazo mengi lakini ghafla zikasambaa taarifa kuwa kuna mwanaume na mwanamke ambao walizisaliti ndoa zao na kwenda kujivinjari gesti, walinasiana wakiwa katika tendo la usaliti.
Uvumi huo ulisambaa kwa kasi eneo hilo na kusababisha umati kujazana Kituo cha Afya cha Chalinze, mkoani hapa ambapo watu hao walionasiana walidaiwa kupelekwa kwa ajili ya huduma ya kwanza.
“Umati ulizidi kuongezeka kila muda ulivyokwenda na kusababisha polisi kuutawanya kwa kutumia mabomu ya machozi ili shughuli za kituo hicho ziweze kuendelea pasipo usumbufu,” alisema shuhuda huyo.
Shuhuda huyo aliongeza kuwa kutokana na kuzagaa kwa uvumi huo ambao hata hivyo baadaye ulibainika kuwa hauna ukweli wowote, paparazzi na mpiga picha huyo naye aliaga nyumbani kwake kuwa anakwenda kushuhudia tukio hilo lakini baadaye walishangaa kusikia amejinyonga.
“Ukweli tulishangaa sana, kwani jamaa alituaga anakwenda kushuhudia tukio hilo kama mpiga picha wa kujitegemea lakini sijui nini kilimtokea ghafla tunasikia amejinyonga!
“Yaani ni tukio la kushangaza sana kila mtu anazungumza lake kuhusiana na tukio hili hakuna anayeamini kama Mogela amejinyonga,” alisema shuhuda huyo.
Gazeti hili lilizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi, (ACP) Jonathan Shana ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema chanzo chake bado hakijafahamika na wanaendelea kufanya uchunguzi.
“Ni kweli hilo tukio limetokea pale Chalinze lakini sababu ya huyo mpiga picha kujinyonga bado haijafahamika kwa kuwa hakuacha ujumbe wowote hivyo tunaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho,” alisema Kamanda Shana.
Mmoja wa ndugu wa marehemu huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini, alisema marehemu alizikwa Ijumaa iliyopita kijijini kwao, Matombo mkoani Morogoro.
Stori: Richard Bukos na Issa Mnally, Pwani
Comments
Post a Comment