Mawakili wamgomea Tundu Lissu
MAWAKILI WA KUJITEGEMEA WAKITOKA MAHAKAMNI BAADA YA KUMALIZA SHUGHULI
ZAO KATIKA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU JIJINI DAR ES SALAAM JANA.
MAWAKILI wa kujitegemea wamekaidi kutii wito wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Mawakili (TLS) wa kutohudhuria mahakamani kwa siku mbili baada ya jana kujitokeza katika mahakama mbalimbali kutetea wateja wao.
MAWAKILI wa kujitegemea wamekaidi kutii wito wa Baraza la Uongozi wa Chama cha Mawakili (TLS) wa kutohudhuria mahakamani kwa siku mbili baada ya jana kujitokeza katika mahakama mbalimbali kutetea wateja wao.
Jumapili, baraza hilo kupitia Rais wa TLS, Tundu Lissu, lilitangaza maazimio matano likiwamo la kuwataka mawakili wote nchini kutohudhuria mahakamani na kwenye mabaraza kwa siku mbili, jana na leo, ikiwa ishara ya kupinga kuvamiwa na kulipuliwa kwa bomu kwa ofisi ya kampuni ya uwakili ya IMMMA jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.
Mawakili jana walionekana kukaidi wito huo baada ya kuhudhuria mahakamani huku wakipinga vikali kauli ya Rais huyo wa TLS.
Akizungumza na Nipashe mjini Dodoma, Mwenyekiti wa TLS Dodoma, Steven Kuwayawaya, alisema mawakili wengi wenye kesi za wateja wao, walihudhuria mahakamani jana, siku ya kwanza ya mgomo uliotangazwa na uongozi wa juu wa chama chao.
"Tuliona ingekuwa vyema mgomo ungeshirikisha mahakama kuwa kitu kimoja maana mahakama inaendeshwa na 'laywers' (wanasheria). Tukigoma ina maana tunagomea mtu ambaye hahusiki na kuwagomea wateja wetu," alisema Kuwayawaya.
Alisema TLS walikubaliana likiwapo jambo kubwa linalohitaji mawakili kwa umoja wao ni lazima baraza la uongozi likutane na 'Chamber of Convenience' lakini haikufanyika.
"Imetuchanganya tunamgomea nani, na ili iweje?" alihoji.
Jijini Dar es Salaam, Nipashe ilipita katika mahakama za Temeke, Kisutu, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani na kukuta mawakili wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.
Baadhi ya mawakili ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini, kwa nyakati tofauti, walihoji sababu za kufanya mgomo huo kuna maslahi gani kwa waajiri wao ambao ni washtakiwa, walalamikaji na walalamikiwa.
"Mimi sijaajiriwa na Lissu, nina mabosi wangu walioniajiri, nagoma ili iweje na kwa mwajiri wangu nitamweleza nini?" alihoji mmoja wa mawakili waandamizi wa kujitemea.
Mtaalamu huyo wa sheria aliongeza: "Halafu tamko la mgomo si halali kwa sababu hatuwezi kuisusia mahakama kufanya kazi, sisi kama maofisa wake.
"Mimi nikigoma leo wakati mawakili kutoka ofisi iliyolipuliwa IMMMA wamekwenda Mahakama Kuu na mahakama nyingine kuwawakilisha wateja wao, sasa sisi wengine tunagoma kwa kumfaidisha nani?"
Wakili mwingine mwandamizi aliyezungumza na Nipashe jijini jana, alisema wao kama chama walitakiwa kuwa watulivu ili kupisha uchunguzi wa Jeshi la Polisi na kwamba suala la kufanya mgomo si wakati sahihi.
"Ni kweli tunalaani tukio lililotokea dhidi ya Kampuni ya Immma lakini tulitakiwa kuwa wapole kwanza ili kupisha uchunguzi...
Jumapili iliyopita alikuja mteja kwangu akaniletea tiketi ya ndege na posho ya kwenda kufanya kazi Arusha sasa leo (jana) nikimweleza TLS imetangaza mgomo, nitakuwa sina akili kwa kweli," alisema wakili huyo baada ya kutoka kusikiliza kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Aidha, alisema mgomo huo unamhusu Lissu peke yake na kwamba atakuwa na sababu zake binafsi ambazo hazihusishi TLS kwa kuwa mawakili karibia wote wako kazini.
Kadhalika, jana majira saa mbili asubuhi Nipashe ilifika katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke jijini na kushuhudia mawakili wa kujitegemea wakiingia katika viunga hivyo kwa ajili ya kuendelea na kesi.
Hali hiyo ilikuwa sawa na Mahakama Kuu na Divisheni zake, Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini.
Source: Nipashe
Comments
Post a Comment