JAJI MKUU, POLISI WATOA ONYO MGOMO WA MAWAIKILI NCHI NZIMA
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Jeshi la Polisi nchini,
wamelionya Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS),
kutoingilia vyombo vya uchunguzi na upelelezi, vinavyochunguza tukio la
mlipuko, uliotokea kwenye ofisi za Kampuni ya Mawakili ya IMMMA usiku wa
kuamkia juzi jijini Dar es Salaam.
Profesa
Juma jana alisema TLS hawana haki ya kutoa agizo kwa mawakili,
kutohudhuria mahakamani na kwenye mabaraza mengine, kwa kuwa kila wakili
ana mkataba binafsi na mteja wake.
Profesa Juma alisema uhuru wa mahakama ni pamoja na kuheshimu mamlaka nyingine za nchi zinapokuwa zinafanya kazi zake.
Alisema
kwa kuwa tukio la kulipuliwa kwa ofisi za Mawakili wa Immma ni tukio la
kihalifu, hivyo wanasheria waiache Polisi na vyombo vingine vya
upelelezi kufanya kazi yao.
“Kama
kutatokea wateja watakaolalamika kuwa mawakili wao hawakufika
mahakamani siku ya Jumanne na Jumatano, hatua za kisheria dhidi ya
mawakili hao zitachukuliwa ikiwemo kuwapeleka kwenye Kamati ya Maadili
ya Mawakili,” alieleza Kaimu Jaji Mkuu.
Kwa upande wao, Jeshi la Polisi limesema liachwe liendelee na kazi ya uchunguzi, badala ya kulihusisha na tukio hilo.
Msemaji
wa Jeshi hilo Makao Makuu, Kamishina Msaidizi Barnabas Mwakalukwa
alisema Jeshi la Polisi ndicho chombo chenye mamlaka ya kufanya
uchunguzi na hivyo kama kuna mtu yeyote mwenye taarifa yoyote kuhusu
tukio hilo, anatakiwa kuzitoa polisi badala ya kuzungumza na vyombo vya
habari.
Kauli
hizo za Polisi na ya Kaimu Jaji Mkuu, zimekuja baada ya Rais wa TLS,
Tundu Lissu kuwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa Baraza
lao la Uongozi lina taarifa kuwa kikundi cha watu wenye silaha za moto,
wakiwa wamevalia sare za Jeshi la Polisi, kiliwateka nyara walinzi
binafsi wa Kampuni ya IMMMA na kuingia ndani ya eneo la ofisi hizo.
Lissu
alidai watu hao baada ya kuingia ndani, walitega milipuko na madumu
manne ya mafuta ya petroli katika maeneo kadhaa ya jengo la ofisi hizo.
Alidai
muda mfupi baadaye, milipuko hiyo ililipuka na kusababisha uharibifu
mkubwa wa jengo la ofisi za IMMMA Advocates zilizoko Upanga pamoja na
majengo jirani.
“Kama
Lissu ana hizo taarifa alitakiwa azilete polisi kwa kuwa ndicho chombo
cha uchunguzi badala ya kuzungumza na vyombo vya habari.
“Kazi
ya polisi ni kufanya uchunguzi wa kina na ndiyo maana Kaimu Kamanda wa
Kanda Maalumu alisema atatoa taarifa uchunguzi ukikamilika, hivyo watu
wanapaswa kusubiri taarifa kamili, nje ya hapo tunakuwa tunafanya kazi
nje ya utawala wa sheria,” alieleza Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mwakalukwa.
Mwakalukwa
alivitaka vyombo vya habari, kuwatafuta walinzi hao ambao Lissu alidai
walitekwa na watu wanaodhaniwa kuwa polisi ili waeleze tukio lilivyokuwa
na ikibidi walinzi hao kutoa taarifa za kutekwa kwao polisi.
Alisema
jambo hilo siyo dogo, hivyo watu waviache vyombo vya uchunguzi,
viendelee na kazi yake kwani uchunguzi pekee ndiyo utakaobaini chanzo na
wahusika.
Ili
kuonesha mshikamano, Baraza la Uongozi la TLS limewataka mawakili wote
ambao ni wanachama wao nchini, wasuse kuhudhuria mahakamani na kwenye
mabaraza ya aina zote kwa siku mbili, kesho na keshokutwa.
Comments
Post a Comment