Dokta Avamiwa Usiku, Achinjwa Babati


Dk. Izack Daniel enzi za uhai wake.
DUNIA haina huruma! Ndiyo kauli unayoweza kuitoa baada ya hivi karibuni mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Dk. Izack Daniel, mkazi wa Ngarenaro, Babati mkoani Manyara, kukutwa akiwa amechinjwa kama kuku chumbani kwake na watu wasiojulikana.

Chanzo makini kililieleza Uwazi kuwa, siku ya tukio, dada wa kazi wa Dokta Izack alitaka kuingia chumbani kwa bosi wake huyo kwa ajili ya kufanya usafi asubuhi.
Lakini tofauti na siku nyingine, ilielezwa kuwa, aligonga mlango kwa muda mrefu bila kufunguliwa hivyo aliamua kwenda kugonga dirishani.

Ilidaiwa kuwa, hata dirishani nako hakukuwa na majibu ambapo baadaye familia ilipigwa na butwaa baada ya kuona damu zikichuruzika kutoka chumbani hadi sebuleni kupitia chini ya mlango.
“Mkewe alikuwa amesafiri hivyo pale nyumbani Dokta Izack alikuwa na wafanyakazi tu na nyumba aliyokuwa amelala ni tofauti na ile wanayolala wafanyakazi.

“Siku ya tukio, dada wa kazi alikwenda kwa ajili ya usafi, akagonga mlango na dirisha la bosi wake huyo, lakini kukawa hakuna majibu.
“Kukaa kidogo, wakapigwa na butwaa kuona damu imetapakaa sebuleni kutoka chumbani.
“Baada ya kuona hali hiyo, wale wafanyakazi na wanafamilia wengine walitoa taarifa polisi ambao walifika na kukuta baba huyo akiwa amechinjwa shingoni kama kuku na damu nyingi kutapakaa chumbani kwake.

“Kiukweli ni tukio la kusikitisha mno,” kilisema chanzo hicho ambacho ni mmoja wa wanafamilia.
Baada ya kupata habari hiyo, Uwazi lilimtafuta mtoto wa mdogo wa marehemu aitwaye Daniel ambaye alikiri baba yake mdogo kuuawa huku akieleza kuwa wameliachia jeshi la polisi kushughulikia suala hilo kwani lipo mikononi mwao.

“Ni kweli ila siku ya tukio nilikwenda na kukuta mwili umeshaondolewa na kilichokuwa kimebaki ni damu nyingi iliyokuwa imetapakaa chumbani,” alisema Daniel.
Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Francis Massawe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na jeraha la kuchinjwa kwa kitu chenye ncha kali shingoni upande wa kushoto.
“Siwezi kueleza kwa undani sana maana nipo barabarani ila alikuwa na jeraha la kuchinjwa shingoni na kitu chenye ncha kali,” alisema Kamanda Massawe.
source:GPL

Comments

Popular posts from this blog