Mama aliyenaswa bila nguo ‘Airport’ Dar, Mapya yaibuka
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipunguni Banana, Praxeda Mkandara, ndiye aliyeanza kufichua undani wa kile kilichojiri baada ya kuiambia Nipashe katika mahojiano naye jana kuwa hakika, ni Mungu ndiye ajuaye juu ya uhai wa mama huyo kwa sababu alikuwa katika hatari kubwa ya kuumizwa vibaya na pia hata kuchomwa moto na wananchi walioshtushwa na tukio hilo.
Alisema badala ya tuhuma za uchawi zinazoenezwa dhidi ya mama huyo ambaye mtaani kwao ni maarufu, ukweli alioupata kutokana na kauli yake mwenyewe ni kwamba alikuwa amevuliwa nguo na mtu aliyekuwa akidaiana naye siku nyingi na kuachwa eneo hilo.
Alisema katika maelezo ya mama huyo, ni kwamba yeye si mchawi na hakuwa akifanya uchawi eneo hilo, bali kuna mtu aliyekuwa akimdai siku nyingi alikutana naye mahala hapo na ndiye aliyemvua nguo kwa nia ya kumdhalilisha.
Awali, mengi yalielezwa kuhusiana na sababu za mama huyo kukutwa akiwa hana nguo na kuhusishwa vitendo hivyo na imani za kishirikina, hasa kutokana na vitu kadhaa vya kiasili alivyokutwa navyo na pia kuonekana kwake akiketi juu ya ungo.
Baadhi ya kile kilichokuwa kikielezwa na watu mbalimbali, wakiwamo walioibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii ni pamoja na madai kwamba mama huyo alikuwa amechanganywa na mambo mbalimbali ya kimaisha kiasi cha kujikuta akienda kwa mganga wa kienyeji na kushawishiwa kufanya aliyofanya kwa matarajio ya kumaliza shida zake mbalimbali, ikiwamo mrundikano wa madeni.
Hata hivyo, hakuna chanzo chochote huru kilichothibitisha ukweli wa taarifa hizo.
Katika mahojiano yake na Nipashe, Praxeda alieleza kuwa baada ya mwanamke huyo kuonekana amefanya kioja kwa kuketi barabarani bila nguo, (yeye) alipigiwa simu na majirani na kuambiwa kuwa mkazi mwenzao huyo wa mtaani kwake amekamatwa akiwa hana nguo katikati ya barabara.
“Nilipigiwa simu nikaambiwa nije haraka yuko uchi wa mnyama. Nikauliza imekuwaje? Nikaambiwa nije mwenyewe kushuhudia. Ikabidi niwaambie wajumbe wangu…mara nikapokea simu nyingine, nikaambiwa fanya haraka watu wanataka kumchoma moto. Hapo ikabidi tukimbilie eneo la tukio,” alisema Praxeda.
Alisema wakati akiwa njiani kufuatilia tukio hilo, alitoa taarifa kituo cha polisi kwa sababu umati wa watu ulikuwa ukiongezeka na hivyo isingekuwa rahisi kumtoa mikononi mwa wananchi hao waliokuwa wakimzonga na kutaka kumuadhibu.
“Polisi walifika na kumchukua. Wakampeleka kituo cha polisi Stakishari na alipofika huko, akaanza kujitetea kuwa yeye siyo mchawi, bali kulikuwa na mtu anayemdai na alipokutana naye pale ndipo alipomvua nguo zake,” alisema Praxeda.
Akisimulia zaidi, Praxeda alisema mwanamke huyo aliwaambia polisi kuwa baada ya kukutana na mdeni wake walianza kuzozana na wakaanza kupigana na ndipo mwenzake huyo akaanza kumuita mchawi, hali iliyosababisha watu kufurika kutaka kujua kuna nini.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa polisi walimuandikia PF3 na wakampa na RB kwa ajili ya kwenda kumtafuta mtu aliyegombana naye kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
“Alisema polisi walimpa maelekezo kuwa mjumbe wa serikali ya mtaa aende naye mpaka kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa ili wachukue hiyo RB wampatie ushirikiano. Mjumbe alimleta ofisini pamoja na RB yake pamoja na PF3, nikamuuliza huyu unayesema unamdai je, unamjua anapoishi? Akajibu ndiyo najua anapoishi.
“Nikamwambia kwa sababu umepewa PF3, nenda kajitibie urudi kesho,” alisema
Alisema kuwa mwanamke huyo alirejea kesho yake na akamuuliza kama ametumiwa picha na watu waliokuwa wakimtazama alipokuwa pale barabarani na alipoonyeshwa alizikataa na kudai kuwa zimetengenezwa.
“Alikataa kuwa zile picha siyo yeye. Nikamwambia unakumbuka jana ulikuja ofisini kwangu ukiwa umeshika ungo na hiyo pochi ukiwa umefunga kitambaa kichwani, iweje ukatae kuwa siyo wewe… akasema hizi picha zimetengezwa siyo zangu, lakini akaniambia nimtumie hizo picha kwenye simu yake,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa tukio hilo limezua gumzo mtaani kwake kwa kuwa hawakutarajia kutokea yaliyotokea.
Praxeda alisema mwanamke huyo ni mwenye heshima kubwa, akiwa ni mmoja wa watu wanaoonekana kuwa na hali nzuri kiuchumi kulinganisha na watu wengine kwenye mtaa anaoishi kwa zaidi ya miaka 15.
Jana, jitihada za kumpata Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamdani kuelezea undani wa tukio hilo lililozua gumzo kubwa zilishindikana.
ILIVYOKUWA
Jumatano ya wiki hii, mama huyo alionekana akiwa amekalia ungo katikati ya barabara katika eneo la Ukonga Banana, majira ya mchana, huku kichwani akiwa amefunga kilemba cheupe huku sehemu nyingine ya mwili huo ukiwa hauna nguo.
Alikuwa pia na ungo ambao picha za mitandaoni zilimuonyesha akiwa ameukalia kabla ya kuinuka na kufuata nguo zake baada ya watu kuanza kumzonga na kumzomea.
Comments
Post a Comment