Katika hatua isiyo ya kawaida, binti yake Bwana Trump, Ivanka, alikaa
kwa niaba ya baba yake wakati wa kikao kinachohusu Afrika kwenye mkutano
wa nchi tajiri wa G20.
Vikao vya asubuhi vililenga masuala muhimu ya uhamiaji na afya.
Picha iliyowekwa twitter na mmoja wa wapatanishi kutoka Urusi
ilimwonyesha Ivanka Trump akikaa katikati ya Rais wa China Xi Jinping na
waziri mkuu wa Uingereza, Bi Teresa May.
Mwandishi wa BBC katika mkutano huo anasema hakumbuki kuwepo na mipango
kama hiyo hapo zamani na kiongozi wa nyadhifa ya juu kama vile waziri wa
mambo ya nje, ndio aghlabu huchukua nafasi ya Rais.
Bi Trump hakuonekana akishiriki katika mchango wowote kuhusu uhamiaji wa
raia wa Afrika kuelekea Ulaya na afya wakati babake alipokuwa
ameondoka.
Picha ya uwepo wake ilichapishwa katika mtandao wa Twitter na mshiriki
mmoja wa Urusi na kuzua hisia kali katia mitandao ya kijamii.
Baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo walisema kuwa bi Trump
hajachaguliwa wala kukaguliwa sifa zake kama mmiliki wa kampuni ya
fesheni kustahili kukaa katika kikao kama hicho chenye hadhi ya juu ya
kidiplomasia.
Wengine walimkosoa hadharani kwa kuwa miongoni mwa viongozi wakuu baada
ya madai yake katika mahojaino kwamba hujaribu kutojishirikisha katika
siasa.
Bi Trump alikuwa amejiunga na babake kwa mkutano wa awali wa G20 siku ya
Jumamosi kuhusu wanawake, biashara na fedha pamoja na kansela wa
Ujerumani Angela Merkel na Christine Lagarde, mkurugenzi wa hazina ya
fedha duniani IMF.
Wanawake wote watatu hapo awali walikuwa pamoja wakati wa kikao cha G20 kuhusu wanawake mjini Berlin mwezi April.
Wakati huo alimtetea babake kama mtu ambaye anapenda kuzaidia familia kuendelea.
Bwana Trump alirudi baadaye ili kuchukua kiti chake kilichokuwa kati ya
waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na rais wa China Xi Jinping.
Comments
Post a Comment