Zaidi ya wanafunzi 2000 watemwa kidato cha tano
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi) George Simbachawene ametoa idadi
ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na
vyuo vya ufundi kwa mwaka 2017 huku jumla ya wanafunzi 2,999 wakiachwa.
Simbachawene ametoa kauli hiyo leo mjini Dodoma wakati akizungumza na
waandishi wa habari na kusema kuwa ufaulu kwa mwaka huu umeongezeka kwa
asilimia 3.75 ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2015.
Waziri amedai kati ya wanafunzi 96,018 waliofaulu kwa daraja la kwanza
hadi la tatu ni wanafunzi 93,019 tu ndiyo waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha tano na vyuo vya ufundi.
Waziri Simbachawene amesema kuwa jumla ya watahiniwa wote waliofanya
mtihani wa kidato cha nne kwa shule kwa mwaka 2016 ni 349,524 huku
waliofanya mtihani wa kujitegemea ni 47,751 ambapo watahiniwa waliofanya
mtihani wa shule waliofaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu ni 96,018
sawa na asilimia 27.60 ya watahiniwa waliofanya mtihani Tanzania Bara.
Simbachawene alisema kutokana na mwongozo wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia wa Mei 15, 2017 jumla ya wanafunzi 93,019 ndiyo wenye Sifa
za kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kwa kuwa
wamefaulu vigezo vyote vya msingi kama vilivyoaibishwa na Wizara ya
elimu sayansi na teknolojia ambapo kati ya hao 92,998 ni wa shule na
wanafunzi 21 ni wale waliosoma taasisi ya elimu ya watu wazima.
Aidha amewataka wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha
tano kuwasili kwa wakati katika shule walizopangiwa July 17 mwaka huu na
kwamba hakutakuwa na mabadiliko ya shule walizopangiwa.
"Na kama kuna mwanafunzi ambaye hataripoti kwenye shule aliyopangiwa kwa
muda wa siku 14 nafasi yake itachukuliwa na mtu mwingine," alisema
Simbachawene.
Comments
Post a Comment