WAZIRI WA MAMBO YA NDANI AMVAA TUNDU LISSU,AFUNGUKA LIVE
Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ‘amemvaa’ Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu kwamba amejaribu kutengeneza kila aina ya kichaka
kukwamisha jitihada za Rais John Magufuli kupambana na usafirishaji
holela wa madini nje ya nchi bila mafanikio.
Ingawa
Mwigulu hakumtaja jina Lissu moja kwa moja alipokuwa akiwahutubia
wananchi wa Kijiji cha Zinzirigi kilichopo katika Jimbo lake la Iramba
Magharibi pia mkoani Singida juzi, hoja nyingi alizogusia ni zile ambazo
Lissu amekuwa akinukuliwa kuzisema.
Moja ya
hoja hizo ni ile ambayo Mwigulu alisema watu wenye nia mbaya walianza
kusema kuwa Serikali itashtakiwa kwa hatua yake ya kuzuia makontena 277
ya mchanga wenye dhahabu.
“Baadaye
watu haohao walisema tena kwamba mchanga ule ni takataka tu lakini
walipoambiwa wasisafirishe mchanga huo wenye madini walisema wanapata
hasara ya Sh4 trilioni kwa siku.”
Hata hivyo, Acacia walisema wanapata hasara ya dola bilioni moja kila siku.
Pia,
Mwigulu alisema tangu Rais Magufuli alipounda kamati mbili kufuatilia
suala la mchanga huo wa madini, watu hao aliowaita kuwa ni wenye nia
mbaya walianza kutumia majina ya marais wastaafu Jakaya Kikwete na
Benjamin Mkapa kama kichaka ili Serikali iache kufuatilia sakata hilo la
mchanga wa madini.
“Hawa
watu walikuwa wanatuona kama mazuzu hivi. Rais wetu amechukua hatua tena
siyo kwa maneno, kwa vitendo. Tumuunge mkono,” alisema Mwigulu.
Tangu
kuanza kwa sakata hilo la mchanga wa madini, Lissu amekaririwa mara kwa
mara akisema kwamba suala hilo linashughulikiwa kisiasa badala ya
kisheria jambo linaloiweka Tanzania katika hatari ya kushtakiwa na
kushindwa.
Pia
alikaririwa bungeni akisema Rais Kikwete anaponaje katika sakata hilo na
jana alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Nchemba alisema msimamo wake uko
palepale kuhusu sakata hilo.
Alichosema Mwigulu
Mwigulu
aliwaeleza wananchi hao kwamba viongozi wa Tanzania hawajawahi kuwa
mawakala wa wale wanaoliibia Taifa na kwamba Watanzania wamewaona
mawakala wa wezi hao kwa sababu wanawatetea. “Na mimi nimpongeze Rais
kwa kuuona ule mtego, akafyatua pyaa! Sasa hivi kama ni gari lao matairi
yote, Rais kashayaondoa upepo, yameshalala chini. Maana lile walitaka
kutengeneza mtego, yaani ni kama mtu anayepigwa anatafuta mti ili
ajifiche,” alisema Mwigulu.
Alisema
heshima ya nchi hii kwa viongozi wastaafu waliofanya kazi nzuri ndiyo
inayowafanya viongozi wa Taifa hili wasing’ang’anie madarakani, jambo
ambalo mataifa mengine wameshindwa kufanya.
“Kama leo
una uhakika ukiondoka madarakani unashtakiwa, kwa nini uondoke
madarakani?” alihoji Mwigulu na kusisitiza kwamba alichofanya Rais
Magufuli ni kulinda heshima za viongozi wastaafu.
Aliwataka
wananchi kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli za kulinda rasilimali
za Taifa kwa sababu ndiyo zinazowawezesha kuwapatia maji, barabara za
lami, umeme, elimu bure na dawa.
Lissu ajibu
Akizungumzia
kauli ya Mwigulu kwamba wanajificha kwenye kichaka cha viongozi
wastaafu ili kufifisha jitihada za Rais Magufuli, Lissu alisema ni
ukweli ulio wazi kwamba huwezi kuwataja wahusika wa mikataba mibovu ya
madini bila kurudi nyuma.
“Tunawaacha
kwa sababu hatuwawezi. Kwa sababu wana kinga,” alisema Lissu na
kusisitiza kwamba wanataka kuona wanapata chanzo halisi cha uzembe
uliofanyika na siyo kuonea watendaji wadogo.
Lissu alisema Sheria za Madini na mikataba mingi ilisainiwa miaka ya 1997 na 1998.
Lissu
ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alieleza
kushangazwa na Serikali kuacha kuzungumzia kwamba kampuni ya Acacia
haijasajiliwa badala yake Rais Magufuli amekubali kukaa na wale
anaowaita wezi ili kujadiliana.
Hatua zilizochukuliwa
Tangu
sakata la mchanga wa madini lilipoanza, Rais Magufuli amechukua hatua
kadhaa ikiwa ni pamoja na kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini
Tanzania (TMAA) na ofisa mtendaji mkuu wake na kuagiza viongozi na
watendaji wengine kuchunguzwa na vyombo vya dola.
Ripoti ya
kamati ya pili iliyoongozwa Profesa Nehemiah Osoro imewataja baadhi ya
viongozi waliohusika katika kuingia mikataba tata na kupendekeza
Serikali iwachukulie hatua.
Waliotajwa
kwenye taarifa ya kamati ya pili iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli Juni
12 ni waliokuwa mawaziri katika Wizara ya Nishati na Madini Profesa
Sospeter Muhongo, William Ngeleja, Nazir Karamagi, Daniel Yona na Dk
Abdallah Kigoda ambaye kwa sasa ni marehemu.
Wengine
ni waliokuwa wanasheria wakuu, Andrew Chenge na Johnson Mwanyika;
manaibu wanasheria wakuu Felix Mrema na Sazi Salula; makamishna wa
madini, Paulo Masanja, Dk Dalaly Kafumu na Ally Samaje na wakuu wa idara
ya mikataba, Maria Ndosi Kejo na Julius Malaba.
Akizungumzia
kutajwa kwake katika ripoti ya kamati ya pili, Mbunge wa Sengerema
(CCM), William Ngeleja alisema bungeni kwamba “kutuhumiwa siyo kukutwa
na hatia, maisha yanaendelea.”
Viongozi wengine waliotajwa katika ripoti hiyo hawajajitokeza kuzungumzia suala hilo.
Comments
Post a Comment