WATOTO WA BOSI WA FREEMASON WAFUNGUKA HAYA BAADA YA KIFO CHA BABA YAO
Takriban
miezi miwili baada ya kifo cha aliyewahi kuwa Bosi wa Jamii ya Siri
(Secret Society) ya Freemason kwa Afrika Mashariki, Jayantilial Andy
Chande ‘Sir Chande’, aliyefariki dunia Aprili 7, mwaka huu, watoto wake
wawili wamefunguka mazito juu ya jamii hiyo.
Kabla
ya kupata neno la watoto hao, kufuatia kifo cha Sir Andy, kumekuwa na
maswali mengi juu ya nini kinaendelea kwenye jamii hiyo kwa sasa hivyo Wikienda lilijipa kazi ya kutafuta majibu ya maswali.
NINI KINAENDELEA FREEMASON?
Katika nusanusa yake, Wikienda lilifika
kwenye Hekalu la Freemason lililopo Mtaa wa Sokoine, mkabala na Hoteli
ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro jijini Dar, jirani na Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) na kutaka kujua kinachoendelea kwa kujigeuza mhitaji wa
kujiunga na jamii hiyo.
Gazeti
hili lilipofika mahali hapo mishale ya mchana, hakukuwa na pilikapilika
nyingi zaidi ya mama ntilie aliyekuwa akisubiria wateja wa msosi.
Baada
ya kuona kimya, ‘pandikizi’ wetu alijaribu kuzama ndani, lakini kabla
ya kuvuka geti ambalo lilikuwa wazi kwenye mlango mdogo, alikutana na
mlinzi aliyemhoji alikokuwa anakwenda.
Mlinzi: Haloo unakwenda wapi?
Wikienda: Samahani, nataka kuingia ndani kuulizia ‘process’ za kujiunga na Freemason, kwani hapa si ndilo hekalu lao?
Mlinzi: Ndiyo ni hapa, lakini hakuna shughuli ya watu kujiunga kwani nani amekuambia watu wanajiunga?
Wikienda: Sasa kwa mtu anayehitaji kujiunga inakuwaje?
Mlinzi: Hapa
hakuna hilo zoezi na wala hakuna mtu aliyewahi kuja hapa akaunganishwa
na Freemason. Kama yupo, huyo alitapeliwa tu maana mjini shule.
Wikienda: Inamaana wenyewe hawapo au?
Mlinzi: Wenyewe hawapo, mara ya mwisho sikumbuki vizuri labda ilikuwa mwezi wa tatu, lakini kuanzia mwezi ujao (wa saba) watakuwepo.
Wikienda: Sasa kama hivi nataka kujiunga, inakuwaje?
Mlinzi: Kwanza unataka kujiunga na nini na ili iweje?
Wikienda: Nataka
kujiunga na Freemason. Nasikia watu waliojiunga wanapata pesa nyingi na
mimi ninazitaka bwana au wewe hutaki pesa ndugu yangu?
Mlinzi: Kweli
wajinga ndiyo waliwao, yaani pamoja na ujanja wote unaamini kuna pesa
za hivihivi bila kufanya kazi? Nimekuambia hapa hakuna ishu ya watu
kujiunga wala sijawahi kuona watu wanakuja tu na kuunganishwa. Kama
nilivyokuambia, kama kuna mtu aliunganishwa kwa kuja tu hapa ujue
alitapeliwa.
Wikienda: Sasa, mbali na hapa, naweza kujiungia wapi kwingine?
Mlinzi: Mimi
kwa hapa sijui, lakini nasikia makao yao makuu kwa Afrika Mashariki
yapo Mombasa (Kenya). Sasa kama unataka uende huko kama una uwezo,
lakini kwa hapa hakuna kitu kama hicho. Kwanza ninavyojua mimi, hayo ni
mambo ya siri. Huwezi kuja hapa tu, ukasema unataka kujiunga, kivipi?
Baada
ya mazungumzo hayo, mlinzi huyo alitaka kuwa mkali kwa kumuona
pandikizi wetu kuwa ni ‘bogas’ hivyo pandikizi huyo aliondoka kwa
maelezo kwamba, hakuna zoezi la watu kuunganishwa mahali hapo.
TURUDI KWA WATOTO WA SIR CHANDE
Katika
mazungumzo yao na waandishi wetu, watoto wa Sir Chande, Manish
Jayantilial na Rupean Jayantilial walieleza kinachoendelea kwenye jamii
hiyo.
Manish
alisema kuwa, kwa upande wake, yeye ni muumini wa Jumuiya ya Freemason
kwa muda mrefu na malengo yake ni siku moja kuwa kiongozi mkubwa wa
jamii hiyo.
“Ni
jambo zuri mno, ni jamii ya watu wanaosaidiana duniani, nimekuwa member
(mwanachama) wake kwa muda mrefu sana na ninatamani siku moja niwe
kiongozi wake mkubwa,” alisema Manish kwa lafudhi ya Kihindi.
MIAKA MITATU BILA MAFANIKIO
Kwa
upande wake, Rupean alikiri jamii hiyo kuendelea na shughuli zake
mbalimbali duniani ikiwemo hapa nchini na kwamba anatamani mno kujiunga
na Freemason.
Rupean
alisema kuwa, kwa muda wa miaka mitatu sasa, amekuwa akifanya maombi ya
kujiunga bila mafanikio lakini anaamini ipo siku naye atafuzu kama
ndugu yake, Manish.
Alisema
kuwa, sababu ya kushindwa kufuzu ni kwamba, bado hajatimiza masharti
yanayotakiwa lakini anaamini siku akiyatimiza atakuwa mwanachama wake.
WALIVUTIWA NA BABA YAO
Manish
na Rupean walisema kuwa, baba yao ndiye aliyewavutia kujiunga na
Freemason kwa kuwa ni jambo zuri kuwa na jamii ya kusaidiana na
kuwasaidia wenye shida mbalimbali kwa kujitolea.
Hata hivyo, walimalizia kwa kusema kuwa, mbali na Tanzania, pia wanaishi nchini Canada na India.
Sir
Chande ambaye mwili wake ulichomwa moto kwenye Makaburi ya Baniani
yaliyopo Makumbusho jijini Dar aliacha watoto watatu na wajukuu watatu.
Comments
Post a Comment