RC ANNA MGHWIRA AMKALIA KOONI FREEMAN MBOWE
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa hatua zilizochukuliwa
na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gellasius Byakanwa za kuondoa miundombinu ya
umwagiliaji katika shamba la Kilimanjaro Veggies si za kisiasa bali ni
taratibu za kisheria za kulinda vyanzo vya maji.
Mghwira alitoa kauli hiyo jana alipotembelea shamba hilo lililopo Kijiji
cha Nshara ili kujionea hali ya uharibifu wa mazingira uliofanywa
katika shamba hilo linalomilikiwa na Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa
CHADEMA, Freeman Mbowe.
“Sheria iko wazi, inasema tusifanye shughuli zozote za kibinadamu zenye
madhara kwenye vyanzo vya maji ndani ya mita 60 kwa mujibu wa sheria na
shughuli hii ina madhara makubwa kwa mazingira na hata kwa binadamu,”
alisema Mghwira.
“Shughuli hii nzuri na ni uwekezaji mkubwa. Ninavyofahamu kilimo cha
strawberry kikishatema maji lazima yaende mahali hata kama unatumia
umwagiliaji wa kisasa wa matone. Maji yanakuwa na madhara kwa binadamu
wanayoyatumia.”
Mghwira alisema kuwa licha ya mmiliki wa shamba hilo kukubaliana na mkuu
wa wilaya kuwa amevunja sheria na angeondoa mazao yake ifikapo Mei 23
mwaka huu, hakufanya hivyo na badala yake alianza kulima mazao mapya.
Imeelezwa kuwa Mbowe alishawahi kuomba viongozi wa mkoa katika kikao cha
RCC kuitishwa kikao ambacho kitajadali masuala ya mazingira na umuhimu
wa kuheshimu umuhimu wa mazingira. Kikao hicho kilifanyika lakini RC
akasema anashindwa kuelewa kwanini Mbowe ameshindwa kuheshimu.
Akizungumzia uharibifu huo, Mbowe alisema kuwa kwa sasa vijana zaidi ya
100 wamepoteza ajira lakini pia anajadiliana na wanasheria wake kuona
nini kinafanyika kutokana na hatua hiyo aliyoiita ya uonevu wa serikali.
Chanzo: Mwananchi
Comments
Post a Comment